DRC yataka utekelezwaji azimio 2773 na kuondolewa vikosi vya Rwanda
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i142194-drc_yataka_utekelezwaji_azimio_2773_na_kuondolewa_vikosi_vya_rwanda
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), imetoa tena wito kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UNSC) kubadili matamshi yake kuwa vitendo ili kukomesha mgogoro uliopo mashariki mwa nchi hiyo.
(last modified 2026-10-15T02:50:35+00:00 )
Oct 15, 2026 02:49 UTC
  • DRC yataka utekelezwaji azimio 2773 na kuondolewa vikosi vya Rwanda

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), imetoa tena wito kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UNSC) kubadili matamshi yake kuwa vitendo ili kukomesha mgogoro uliopo mashariki mwa nchi hiyo.

Mwakilishi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ametoa wito huo katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kusisitiza kwamba, kuna haja ya  kutekelezwa kikamilifu Azimio namba 2773 hasa kuondolewa kabisa majeshi ya Rwanda katika ardhi ya DRC, kusitishwa msaada unaotolewa kwa kundi la AFC/M23 na kuheshimiwa kikamilifu mamlaka ya kitaifa na mipaka ya nchi hiyo.

Akizungumza kwenye mkutano kuhusu hali ya ukanda wa Maziwa Makuu, mwanadiplomasia wa DRC amepongeza ripoti ya Mjumbe Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, lakini akabainisha kuwa, mapigano, kukaliwa kwa baadhi ya vijiji, na mateso ya raia bado vinaendelea licha ya kuwepo kwa juhudi za kidiplomasia."

Kwa mujibu wa Kinshasa, wakati wa ahadi umekwisha; sasa ni wakati wa utekelezaji mzuri wa ahadi zilizotolewa na pande mbalimbali na maamuzi ya Baraza la Usalama.

Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (RDC) imeweka wazi msimamo wake kwamba, mipaka yake, usalama wake, na haki yake ya kujitawala kama taifa huru ni mambo ambayo hayawezi kuwekwa mezani kwa ajili ya mashauriano au makubaliano yoyote na pande za nje.

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo imekuwa ikimtuhumu jirani yake Rwanda kuwa inaliunga mkono kundi la waasi wa M23, madai ambayo yanakanushwa na Kigali, lakini yanaungwa mkono na Marekani, Ufaransa, Ubelgiji na wataalamu wa Umoja wa Mataifa.