Rais Pezeshkian: Mabomu na makombora hayawezi kuilazimisha Iran isalimu amri
-
Rais Masoud Pezeshkian wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran
Rais Masoud Pezeshkian amesema kuwa mabomu na makombora hayawezi kuilazimisha Iran kujisalimisha, wakati Marekani ikiendelea kutoa vitisho vya maneno dhidi ya taifa hilo, kufuatia kushindwa kwake kuipigisha magoti Jamhuri ya Kiislamu kupitia mashambulizi ya kijeshi na vikwazo.
“Mabomu na makombora hayawezi kulazimisha taifa kujisalimisha, lakini tukigawanyika ndani ya nchi yetu, adui atafikia lengo lake,” amesema Pezeshkian siku ya Alhamisi, wakati wa hafla ya kuadhimisha Siku ya Taifa ya Wauguzi.
Pezeshkian pia ameonya kuhusu njama za maadui za kutumia migawanyiko ya ndani na matatizo yaliyopo nchini humo, kwa lengo la kudhoofisha nguvu na umoja wa Iran.
Aidha, Pezeshkian amesisitiza kuwa wananchi wa Iran wameamua kusimama imara mbele ya wapinzani wao, ambao wanaendelea kuongeza shinikizo dhidi ya nchi hiyo kwa kutumia njia mbalimbali, zikiwemo vikwazo katika njia za usafirishaji na mawasiliano.
“Adui aliamini kuwa upungufu wa umeme, maji na gesi, matatizo ya mafuta, changamoto za kimazingira, matatizo ya sekta ya benki, nakisi ya bajeti na changamoto za mifuko ya pensheni vingesababisha jamii ya Iran kugawanyika. Hata hivyo, uvumilivu na mshikamano wa wananchi umeonesha kuwa matarajio hayo hayakuwa sahihi,” aliongeza.
Wakati huohuo, Rais wa Iran amesifu kujitolea kwa wauguzi wa Iran na wahudumu wengine wa afya, pamoja na wale waliosimama imara katika mazingira magumu zaidi ili kulinda usalama wa nchi na umoja wa mipaka yake.
Aidha, Pezeshkian amewataka viongozi kujiepusha na kauli au vitendo vinavyoweza kudhoofisha umoja wa kitaifa, na kuwataka kutumia rasilimali zote zilizopo ili kuimarisha imani ya wananchi kwa viongozi na taasisi za nchi.
Marekani na Israel zilianzisha vita vya uchokozi dhidi ya Iran Februari 28.
Siku 40 baadaye, Aprili 8, Marekani ilitangaza usitishaji wa mapigano, kufuatia muqawama wa Iran na operesheni zake za kulipiza mashambulizi zilizofanikiwa.