Umoja wa Mataifa waonya kuhusu athari za mapigano mapya Tigray, Ethiopia
Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, ameonya kuhusu athari za ongezeko la mapigano nchini Ethiopia.
Volker Türk ameeleza kuwa, raia wanakabiliwa na hatari kubwa kutokana na mapigano mapya yaliyoibuka hivi karibuni nchini Ethiopia kati ya wanajeshi wa serikali na wapiganaji wa TPLF kwenye eneo la Tigray.
Afisa huyo wa Umoja wa Mataifa ametoa wito kwa pande zote zinazohusika na mzozo huo kupunguza mvutano na kuepusha nchi hiyo kurejea kwenye vita kamili.
Taarifa hiyo imesema ripoti zinaonyesha mashambulizi ya anga yaliyofanywa na jeshi la Ethiopia, baadhi yakitumia droni, yalilenga shule tano katika eneo la Tigray tarehe 22 Septemba na kusababisha vifo na majeruhi. Mashambulizi ya kombora yameripotiwa pia katika mji wa Kobo, katika mkoa wa Amhara, ambapo raia kadhaa wameuawa.
Hayo yanajiri katika hali ambayo, wakazi wa Mekelle, makao makuu ya Tigray, wakisema wanaishi katika hali ya hofu na wahka huku mapigano yakizidi kushika kasi.
Wakati huo huo, Jeshi la Ulinzi wa Taifa la Ethiopia limetangaza kuwa, waasi 272 wa kundi la Tigray People's Liberation Front (TPLF) waliuawa wakati waasi hao walipofanya shambulio la mapinduzi na kukabiliwa na majibu makali ya jeshi usiku wa Jumanne.
Matukio ya hivi karibuni yamezua hofu ya uwezekano wa kurejea mgogoro wa umwagaji wa damu, hasa ikizingatiwa kwamba vita vya miaka miwili kati ya wanajeshi wa serikali ya shirikisho la Ethiopia na wapiganaji TPLF vilivyoanza tangu mwezi Novemba 2020 hadi Novemba 2022 vilisababisha vifo vingi mbali na wimbi la wakimbizi na uharibifu wa mali.
Mgogoro huo wa miaka miwili uliacha mamilioni ya watu wakihitaji misaada ya dharura ya kibinadamu kabla ya pande hizo mbili kutia saini makubaliano muhimu ya amani ya Pretoria nchini Afrika Kusini na kukomesha mapigano baina yao.