Wapiganaji wa TPLF wadhibiti uwanja wa ndege wa kanda ya Tigray, Ethiopia
Wapiganaji wa Harakati ya Ukombozi ya Watu wa Tigray, Tigray People's Liberation Front (TPLF), iliyoko kaskazini mwa Ethiopia, wameripotiwa kuwa wameudhibiti uwanja wa ndege katika mji mkuu wa kanda hiyo. Hayo ni kwa mujibu wa ripoti zilizotolewa jana Jumatano na vyanzo vya kiusalama katika eneo hilo.
TPLF, ambao wanadhibiti kanda hiyo, walipigana katika vita vya wenyewe kwa wenyewe dhidi ya serikali kuu mwaka 2020-2022 vilivyosababisha vifo vya watu karibu 600,000, kulingana na makadirio ya Umoja wa Afrika.
Mfanyakazi mmoja wa kampuni ya Alula Aba Nega katika mji mkuu wa mkoa wa Tigray, Mekelle ameviambia vyombo vya habari: "tulipokuwa njiani kwenda kazini katika uwanja wa ndege, meneja wetu alimpigia dereva simu na kumwambia kuwa uwanja wa ndege umedhibitiwa na vikosi vya Tigray. Kwa kuwa hakukuwa na ndege, alituambia turudi nyumbani".
Taarifa hizo zilithibitishwa na chanzo kimoja cha usalama cha taifa la kigeni nchini Ethiopia.
Idadi ndogo ya polisi wa serikali kuu wanalinda uwanja huo wa ndege, na hatima yao haikuweza kufahamika.
Rada za ndege, na ufuatiliaji, zilionyesha ndege ya Jumatano asubuhi kutoka Mekelle kuelekea mji mkuu, Addis Ababa, haikuweza kuondoka.
"Shirika la Ndege la Ethiopia limesitisha safari zake za kwenda Mekele, Axum, na Shire kuanzia leo, kutokana na hali ilivyo sasa kanda ya Tigray," ilieleza taarifa iliyotolewa na shirika hilo la taifa la ndege.
Ethiopia inakabiliwa na changamoto kadhaa za kiusalama, ikiwemo katika kanda zake zenye idadi kubwa ya watu, Oromia na Amhara…/