Jeshi la Ethiopia lasonga mbele Tigray, hofu yatanda katika ukanda mzima
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i141972-jeshi_la_ethiopia_lasonga_mbele_tigray_hofu_yatanda_katika_ukanda_mzima
Jeshi la Taifa la Ulinzi la Ethiopia (ENDF) limeendelea kusonga mbele katika jimbo la Tigray lililokumbwa na mzozo, huku hofu ikiongezeka ya uwezekano wa mzozo huo kuenea katika nchi jirani na kuongezeka mvutano mkali wa kidiplomasia.
(last modified 2026-10-06T03:31:32+00:00 )
Oct 06, 2026 03:29 UTC
  • Jeshi la Ethiopia lasonga mbele Tigray, hofu yatanda katika ukanda mzima

Jeshi la Taifa la Ulinzi la Ethiopia (ENDF) limeendelea kusonga mbele katika jimbo la Tigray lililokumbwa na mzozo, huku hofu ikiongezeka ya uwezekano wa mzozo huo kuenea katika nchi jirani na kuongezeka mvutano mkali wa kidiplomasia.

Wakati mapigano yakiendelea kati ya ENDF na washirika wake dhidi ya vikosi vinavyokiunga mkono Chama cha Ukombozi wa Watu wa Tigray (TPLF) katika eneo la kaskazini mwa Ethiopia, serikali ya shirikisho imetangaza kuwa kuna juhudi zinaendelea za kuunda mfumo mpya wa utawala huko Tigray.

Shirika la Habari la Ethiopia (ENA) linalomilikiwa na serikali limetangaza habari hiyo na kusema kuwa, juhudi hizo zitawawezesha watu wa Tigray kujitawala na kurejesha amani na utulivu katika eneo hilo. Sambamba na hayo, mazingira yanaandaliwa ya kufanyika uchaguzi wa jimbo hilo ndani ya miezi michache ijayo.

Shirika hilo la habari limemnukuu Abraham Belay, mkuu wa zamani wa utawala wa mpito ulioteuliwa na serikali ya shirikisho huko Tigray akisema kuwa, kufuatia operesheni hizo, mifumo mipya ya utawala itaanzishwa kuanzia ngazi za chini za maeneo ya ndani kwenda juu na jamii itashirikishwa moja kwa moja.

Amewataka wananchi wote wa Ethiopia kuunga mkono juhudi zinazoendelea za kumaliza kipindi cha mpito na kuruhusu watu wa Tigray kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya taifa.

Jumapili usiku, wakazi wa Tigray walithibitisha kuwa jeshi la Ethiopia na washirika wake, hasa Kikosi cha Amani cha Tigray, walichukua udhibiti wa mji wa Mekelle ambao ndiyo makao makuu ya jimbo la Tigray.

Video zilizoenea kwenye mitandao ya kijamii siku ya Jumapili nazo zilionesha kuwa vikosi vya serikali vimeendelea kusonga mbele zaidi kuelekea kaskazini mwa jimbo la Tigray.

Wataalamu na wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanasema kuwa kufanikiwa jeshi la serikali ya Ethiopia kuyadhibiti Makao Makuu ya jimbo la Tigray kunaashiria awamu mpya ya ongezeko la mapigano kaskazini mwa Ethiopia hasa kwa vile tarehe 20 mwezi uliopita wa Septemba kuliundwa muungano mpya wa makundi saba ya upinzani yenye silaha nchini Ethiopia.