Fadavi: Wamarekani wamekimbia umbali wa zidi ya Kilomita 1,000 kutoka Iran
Aliyekuwa kamanda wa Jeshi la Majini la Walinzi wa Mapinduzi ya KIislamu (SEPAH) ambaye hivi sasa ni mkuu wa timu ya washauri wa Kamanda Mkuu wa jeshi hilo amesema: "Wamarekani wamekimbia umbali wa zaidi ya kilomita 1,000 kutoka kwenye mipaka ya Iran; na hatua hiyo haikutokana na hiari yao wenyewe, bali ni kutokana na nguvu ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran."
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Fars, Brigedia Jenerali Ali Fadavi amesema hayo kwenye mahojiano maalumu ya televisheni na kusema: "Ni jambo la uhakika kabisa kwamba Lango-Bahari la Hormuz limekuwa chini ya udhibiti wa Iran kwa muda mrefu sana."
Ameongeza kuwa: "Wamarekani wana uwezo mkubwa zaidi wa kijeshi wa baharini; ikimaanisha kuwa jeshi lao la majini lina nguvu zaidi kuliko la nchi kavu na angani.
Jenerali Fadavi vilevile amesema: "Wamarekani wamekuwepo katika eneo la Ghuba ya Uajemi kwa miaka mingi, lakini hii ni mara ya kwanza ambapo dunia inashuhudia kwa macho yake kuwa hakuna hata meli moja ya Marekani si katika eneo la Ghuba ya Uajemi, si katika Lango-Bahari la Hormuz, si katika Bahari ya Oman na wala si katika bahari ya kaskazini."
Mkuu wa timu ya washauri wa Kamanda Mkuu wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu SEPAH aidha amesema: "Wanamapambano mashujaa wa Iran wamesimama imara kwa miaka mingi kupambana na 'Shetani Mkubwa' Marekani; na licha ya shetani huyo kuwa na nguvu kubwa za kijeshi, lakini ameshindwa kufikia lengo lolote kati ya malengo yake ya vita."
Jenerali Fadavi amezungumzia pia suala la meli kupita katika eneo la kusini mwa Lango-Bahari la Hormuz na kusema: "Manahodha wa meli wanakataa kupita katika eneo hili, lakini kutokana na masuala ya bima na fedha, pamoja na kukwepa kubeba dhima, huwa hatimaye wanalazimika kupita katika eneo hilo."
Vilevile amesema: "Mara kadhaa Wamarekani wanapojaribu kuingiza meli zao za kijeshi katika Lango-Bahari la Hormuz, wanashambuliwa na Jeshi la Majini la SEPAH pamoja na Kikosi cha Anga na Anga za Juu cha Jeshi hilo la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu, na hivi sasa wamefikia katika hali ambayo hawawezi tena kuendesha vita kama zamani."