Skuli 500 zafungwa Ufaransa, 24 zachomwa moto, maandamano ya wanafunzi yanaendelea
Migomo ya wanafunzi imeendelea kote nchini Ufaransa siku ya Jumatatu, huku masomo yakisitishwa kikamilifu au kwa sehemu katika skuli za sekondari kati ya 400 na 500 kutokana na maandamano ya kulalamikia hali ya elimu na ongezeko la matukio yanayohusiana na suala hilo.
Shirika la utangazaji la BFMTV, limemnukuu Waziri wa Elimu Edouard Geffray, akieleza kwamba idadi hiyo inawakilisha karibu asilimia 10 hadi 13 ya skuli za sekondari 3,700 nchini humo huku akiashiria hofu ya kiusalama katika skuli zilizoathirika.
Migomo hiyo, iliyoanza katika eneo la Paris katikati ya mwezi wa Septemba, ilishika kasi wiki iliyopita huku wanafunzi wakidai rasilimali zaidi, majengo ya skuli yanayotunzwa vyema, madarasa yenye idadi ndogo ya wanafunzi, na hatua za kushughulikia uhaba wa wafanyakazi.
Katika eneo la Ile-de-France linalozunguka Paris, zaidi ya skuli za sekondari 160 zilitarajiwa kufungwa siku ya Jumatatu. Hayo ni kulingana na mamlaka za eneo hilo.
Harakati hizo ziliambatana na matukio kadhaa jijini Paris.
Katika Skuli ya Sekondari ya Vauquelin jijini, mamlaka ziliripoti matukio matatu ya uchomaji moto karibu na lango la kuingilia skulini humo jana asubuhi.
Imeelezwa kuwa, skuli kadhaa "zimeteketezwa kwa moto au kuharibiwa na kuporwa".
Wizara ya Mambo ya Ndani na Wizara ya Elimu zimeripoti ongezeko kubwa la idadi ya watu waliokamatwa na kujeruhiwa tangu maandamano hayo ya shinikizo yalipoanza.
Mamlaka zimesema watu wapatao 5,000 wamekamatwa tangu kuanza kwa vuguvugu hilo, huku asilimia 85 kati yao wakiwa ni vijana walio chini ya umri wa miaka 18 katika eneo la Ile-de-France.
Waziri Mkuu Francois Bayrou anajaribu kutatua mgogoro huo kwa kuwasilisha mapendekezo matano na ametoa wito wa kufikiwa maamuzi kabla ya mwisho wa mwezi huu wa Oktoba…/