Eritrea yavunja uhusiano wake wa kidiplomasia na Ethiopita
Eritrea imetangaza kupitia wizara yake ya mambo ya nje kwamba inavunja uhusiano wake wa kidiplomasia na Ethiopia kujibu hatua ya Ethiopia ya kuwafukuza wanadiplomasia 10 wa nchi hiyo mjini Addis Ababa.
Katika taarifa iliyowekwa kwenye mtandao wa X, wizara hiyo imesema Eritrea “haina chaguo jingine isipokuwa kujibu mapigo kwa hatua kama hiyo na kukata mahusiano yote ya kidiplomasia na Ethiopia, licha ya madhara yote yanayoweza kutokea kutokana na hatua hiyo.”
Ethiopia ilitangaza kuwafukuza wanadiplomasia 10 wa Eritrea, kwa madai kwamba, walihusika katika shughuli ambazo zilikuwa “tishio la moja kwa moja” kwa usalama wa taifa wa Ethiopia na kuwataka wawe wameshaondoka nchini humo ndani ya saa 48.
Uamuzi huo umechukuliwa muda mfupi baada ya serikali ya Addis Ababa kutangaza pia kuwa itafunga ubalozi wake mjini Asmara kwa sababu ya ilichokiita "vitendo vya moja kwa moja na visivyo vya moja kwa moja vya uhasama na uchokozi wa Eritrea dhidi ya Ethiopia".
Wakati huohuo, shirika la utangazaji la Ethiopia linalomilikiwa na serikali limeripoti kuwa, Serikali ya Ethiopia ilitangaza Alkhamisi kwamba mwanadiplomasia mmoja wa Misri ni mtu asiyetakiwa nchini humo na kumuamuru aondoke ndani ya saa 48.
Mkabala wake, Misri nayo imechukua hatua ya kujibu mapigo kwa kumtangaza afisa wa ngazi ya juu katika ubalozi wa Ethiopia nchini humo kuwa mtu asiyetakiwa na kumpa muda wa saa 48 za kuondoka. Hayo yameripotiwa na kituo cha habari cha Al Qahera News, ambacho kina uhusiano na serikali, kikimnukuu afisa mmoja wa nchi hiyo.
Hayo yanajiri, wakati mapigano makali yanaendelea kuripotiwa kati ya vikosi vya serikali ya shirikisho ya Ethiopia na makundi ya upinzani yenye silaha. Siku ya Jumatano na Alkhamisi, miripuko ilisikika katika mji mkuu Addis Ababa, huku wapiganaji wakipambana na vikosi vya serikali katika eneo la kaskazini pia la Afar…/