Watu 17 waaga dunia katika ajali iliyotokea barabara ya Nairobi-Mombasa
-
Watu 17 waaga dunia katika ajali iliyotokea barabara ya Nairobi-Mombasa
Watu wasiopungua 17 wamefariki dunia huku wengine kadhaa wakijeruhiwa baada ya ajali iliyohusisha magari kadhaa kutokea mapema Jumamosi kwenye barabara kuu ya Nairobi-Mombasa huko nchini Kenya.
Kamishna wa Kaunti ya Makueni, Abdullahi Khalif, amesema ajali hiyo ilitokea baada ya dereva wa lori kupoteza mwelekeo wa gari kutokana na hitilafu ya breki kabla ya kugonga magari mengine matano.
Kwa mujibu wa mashuhuda, miongoni mwa magari yaliyohusika ni garia la abiria la matatu lililokuwa likisafirisha waumini wa Kikatoliki waliokuwa wakielekea Subukia, kaunti ya Nakuru, kwa ibada.
Wasamaria wema, maafisa wa uokoaji na polisi walifika eneo la tukio na kuwapeleka manusura katika Hospitali ya Sultan Hamud Sub-County kwa matibabu.
Hospitali hiyo ilithibitisha kuwa baadhi ya majeruhi walitibiwa na kuruhusiwa kuondoka, huku uchunguzi ukiendelea kubaini chanzo hasa cha ajali hiyo.
Kenya inaendelea kukabiliwa na changamoto kubwa ya ajali za barabarani, huku maelfu ya watu wakipoteza maisha kila mwaka kutokana na ajali hizo.
Takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaonyesha kuwa mwaka 2021, Kenya iliripoti vifo 4,579 vilivyotokana na ajali za barabarani. Hata hivyo, WHO ilikadiria kuwa idadi halisi ya vifo ilifikia karibu 14,926, sawa na kiwango cha takribani vifo 28 kwa kila watu 100,000.
Ajali hizo huathiri zaidi watumiaji wa barabara, wakiwemo watembea kwa miguu, waendesha pikipiki, waendesha baiskeli na abiria wa magari ya usafiri wa umma. WHO pia inasema kuwa majeraha yatokanayo na ajali za barabarani ni miongoni mwa sababu muhimu za vifo nchini Kenya, hasa kwa wanaume.
Mamlaka ya Kitaifa ya Usafiri na Usalama Barabarani nchini Kenya, NTSA, ndiyo yenye jukumu la kusimamia usalama wa barabarani, ikiwemo udhibiti wa magari ya usafiri wa umma, ukaguzi wa magari, ukusanyaji wa takwimu na utekelezaji wa mikakati ya kupunguza ajali.