Kwa nini Marekani haiaminiki?
https://parstoday.ir/sw/news/world-i141856-kwa_nini_marekani_haiaminiki
Huku akiashiria historia mbaya ya utawala wa Marekani kukiuka mara kwa mara ahadi zake, Rais Masoud Pezeshkian wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, amesisitiza kuwa Iran haiiamini tena Marekani.
(last modified 2026-10-01T10:34:33+00:00 )
Oct 01, 2026 10:29 UTC
  • Kwa nini Marekani haiaminiki?

Huku akiashiria historia mbaya ya utawala wa Marekani kukiuka mara kwa mara ahadi zake, Rais Masoud Pezeshkian wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, amesisitiza kuwa Iran haiiamini tena Marekani.

Uchambuzi wa historia ya uhusiano wa Iran na Marekani unaonyesha kuwa suala la nchi hiyo ya Magharibi "kukiuka ahadi" zake ni suala la kawaida kabisa, na ni katika tabia na mwenendo wake wa kimkakati, kuanzia kupuuza kinga ya mali za Iran chini ya Makubaliano ya Algiers hadi kujiondoa kwa upande mmoja katika makubaliano ya JCPOA na kushindwa kutimiza wajibu wake chini ya Mkataba wa Islamabad.

Katika mahojiano ya karibuni na shirika la habari la Al Jazeera, Rais Pezeshkian ametaja historia ya nchi hiyo ya kuvunja ahadi zake pamoja na uzoefu wa vita, mashambulizi ya kijeshi, na vikwazo vilivyofuatia mazungumzo ya awali, kama msingi wa msimamo huo wa Tehran. Amesema ingawa Iran haikatai kufanya mazungumzo, lakini haiko tayari kuiamini tena Washington bila kuwepo kwa dhamana na utatuzi kuhusu ahadi zake za awali. Msimamo huu unaakisi kanuni muhimu katika mtazamo wa kidiplomasia wa Tehran. Pezeshkian amebainisha wazi tofauti iliyopo kati ya "mazungumzo" na "kuaminiana." Ingawa mazungumzo bado yanawezekana, lakini kuaminiana hakuko tena kama sharti la awali la kufanyika mazungumzo, na kwamba imani inapaswa kujengwa kupitia vitendo vya Marekani.

Pezeshkian amehoji mantiki ya kukutana na Rais wa Marekani ikizingatiwa kuwa makubaliano ya awali yalishasainiwa lakini Marekani ikashindwa kuyatekeleza. Hivyo, suala si kutofautiana tu kuhusu yaliyomo kwenye makubaliano hayo, bali tatizo la msingi linahusu ukweli wa ahadi za Marekani.

Kwa msingi huo, Rais wa Iran amesisitiza kuwa mazungumzo yoyote yanayoweza kufanyika baadaye lazima yajengwe juu ya makubaliano ya awali na kwamba Marekani lazima iweke wazi msimamo wake kuyahusu. Tehran haitaki mazungumzo yaanze upya kutokea sufuri, kwa sababu mfumo wa makubaliano tayari upo, na kwamba Washington lazima ishughulikie suala la uaminifu katika makubaliano hayo. Uzoefu wa vita pia umezingatiwa katika mlingano huu. Kwa mtazamo wa Tehran, haiwezekani kuzungumzia suala la mazungumzo huku kukifanyika maandalizi ya kutumia vikwazo na mashambulizi ya kijeshi dhidi ya watu wa Iran. Kwa mtazamo wa Iran, mazungumzo yoyote yanayoambatana na vitisho vya kijeshi hayana uhalali wa kisiasa.

Suala la Lango-Bahari la Hormuz lazima lieleweke ndani ya muktadha huo huo. Pezeshkian amesema lango hilo lilifungwa kama hatua ya kukabiliana na mashinikizo yasiyo halali ya Marekani, lakini akasisitiza wakati huo huo kuwa mgogoro uliopo unaweza kutatuliwa kupitia mazungumzo badala ya kutumiwa nguvu. Hii inaonyesha kuwa, ingawa Tehran iko tayari kutumia rasilimali zake za kijiografia na kisiasa kwa ajili ya kukabiliana na vitisho vya adui, lakini inaona diplomasia kama njia pekee ya kutatua mgogoro huo. Ujumbe wa Pezeshkian kwa eneo pia uko wazi: Ghuba ya Uajemi haina haja ya kuwa na "polisi wa kikanda"; usalama wa eneo lazima udhaminiwe na nchi za eneo hili zenyewe. Msimamo huu unapinga moja kwa moja usanifu wa usalama unaotegemea uwepo wa jeshi la Marekani na kusisitiza jukumu la mataifa ya kikanda katika kutatua migogoro ya eneo.

Rais wa Iran pia amepuuzilia mbali majaribio ya Trump ya kujaribu kuchochea tofauti na migawanyiko ndani ya mfumo wa utawala nchini Iran na kusema juhudi hizo hazitafua dafu. Kuashiria kwake mikutano yake ya muda mrefu na Kiongozi Mkuu wa Iran ni jibu madhubuti kwa maadui wanaojaribu kuibua mizozo kati ya vyombo tofauti vya kufanya maamuzi nchini. Kwa kweli, maamuzi makubwa ya kitaifa yanafikiwa ndani ya mfumo maalum uliowekwa, na hata timu zinazofanya mazungumzo na maadui wachokozi pia zinatekeleza majukumu yao ndani ya mfumo huo huo.

Hatimaye, msimamo uliochukuliwa na Rais wa Iran unaashiria mabadiliko makubwa katika mbinu ya Tehran kuhusiana na nchi za Magharibi, ambapo kutokea sasa hakutakuwepo tena na suala la kuwa na mtazamo mzuri wa kidiplomasia kuhusiana na nchi hizo, bali uhalisia wa mambo na uzoefu wa kihistoria ndio utakaofanya kazi. Mazungumzo yoyote ya baadaye yatakuwa na maana tu pale Marekani itakapotekeleza ahadi zake za awali, na pia kuchukua hatua za lazima kwa ajili ya kurejesha imani na uaminifu wake uliopotea kwa taifa la Iran kupitia hatua za kivitendo na zinazoweza kuthibitishwa. Bila kutekelezwa sharti hili la msingi, mazungumzo mengine yatakuwa ni kurudiwa tu mzunguko wa mazungumzo yasiyo na tija. Kwa maneno mengine, ni dhamana gani ya msingi itakayotolewa na Washington ili kukomesha mzunguko huu batili wa mazungumzo, makubaliano, uvunjaji wa ahadi, na kurejea kwenye vikwazo na vita?