Wanajeshi wa Marekani kuondoka nchini Iraq katika muda uliopangwa
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i141822-wanajeshi_wa_marekani_kuondoka_nchini_iraq_katika_muda_uliopangwa
Msemaji wa Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Iraq amesema kuwa, vikosi vya Marekani pamoja na vikosi vya muungano wa kimataifa vitakamilisha mchakato wa kuondoka nchini Iraq tarehe 30 Septemba mwaka huu.
(last modified 2026-09-30T02:56:56+00:00 )
Sep 30, 2026 02:54 UTC
  • Wanajeshi wa Marekani kuondoka nchini Iraq katika muda uliopangwa

Msemaji wa Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Iraq amesema kuwa, vikosi vya Marekani pamoja na vikosi vya muungano wa kimataifa vitakamilisha mchakato wa kuondoka nchini Iraq tarehe 30 Septemba mwaka huu.

Sabah al-Nu’man, msemaji wa Amiri Jeshi Mkuu wa Majeshi ya Iraq, ametangaza kwamba mchakato wa kuondoka kwa vikosi vya Marekani na vikosi vya muungano wa kimataifa nchini Iraq utakamilika kikamilifu leo Jumatano tarehe 30 Septemba.

Pia amesisitiza kwamba hakutakuwa na kikosi chochote cha kijeshi cha kigeni wala kambi ya kijeshi ya kigeni katika ardhi ya Iraq.

Al-Nu’man amesema: “Hali yetu ya kiusalama ni nzuri na tuna udhibiti wa maeneo yote ya Iraq. Hakuna sababu ya kuwa na wasiwasi kuhusu usalama wa nchi, na vikosi vyetu vimetawanyika katika maeneo yote ya Iraq. Uhusiano wetu na muungano wa kimataifa pia utabadilika na kuwa ushirikiano wa pande mbili wa aina tofauti.”

Awali, Waziri Mkuu wa Iraq, Ali al-Zaidi, alisema kwamba tarehe ya kukamilika kwa ujumbe wa muungano wa kimataifa nchini Iraq, iliyowekwa kuwa 30 Septemba, ni tarehe ya mwisho na isiyoweza kubadilishwa.

Januari 5, 2020 Bunge la Iraq lilipiga kura na kupitisha mpango uliopendekezwa na wabunge wa kuhitimisha makubaliano ya kijeshi yaliyofikiwa kati ya nchi hiyo na Marekani na kuwataka wanajeshi wa Marekani waondoke nchini humo.

Upinzani dhidi ya uwepo wa kijeshi wa Marekani nchini Iraq umeendelea kwa miaka kadhaa, huku baadhi ya viongozi wa kisiasa na makundi ya Iraq wakisisitiza kuwa nchi hiyo ina uwezo wa kujilinda bila kutegemea vikosi vya kigeni.