Vita Dhidi ya Iran: Janga la Kimkakati kwa Marekani
Mtandao wa Marekani wa MS NOW umetoa onyo kuhusu madhara ya kiuchumi, kijeshi na kiusalama yanayoweza kutokana na vita vya Marekani dhidi ya Iran. MS NOW imeelezea vita dhidi ya Iran kama "janga la kimkakati" kwa Washington, ikionya kuwa gharama kubwa na endelevu za mgogoro huo zinaweza kuwa sababu kuu ya Chama cha Republican kushindwa katika uchaguzi wa katikati ya muhula wa Bunge la Marekani.
Kama ripoti ya MS NOW inavyoonyesha, vita vya Marekani dhidi ya Iran vinaweza kuvuka haraka mipaka ya mgogoro mdogo wa kijeshi na kuwa janga kamili la kimkakati kwa Washington. Vita hivi havijashindwa tu kufikia malengo yaliyowekwa na Marekani, bali pia vimeathiri vibaya uchumi, uwezo wa kijeshi, hadhi ya kimataifa na nafasi ya chama tawala nchini Marekani. Baada ya kupita zaidi ya siku mia mbili za mapigano, imezidi kudhihirika wazi kuwa gharama za mgogoro huu si za muda mfupi wala hazionekani kwenye uwanja wa vita pekee bali, zimeingia katika maisha ya kila siku ya Wamarekani, masoko ya fedha, mifumo ya usafirishaji na ugavi, na hata uchaguzi wa katikati ya muhula wa bunge.
Kwa upande wa uchumi, ongezeko la takriban asilimia hamsini la bei ya petroli na dizeli tangu vita vilipoanza, kupanda kwa gharama za mafuta ya ndege, jambo ambalo limepelekea kupanda kwa nauli za ndege kwa zaidi ya asilimia ishirini, pamoja na kupanda kwa viwango vya riba ya mikopo ya nyumba, yote hayo yanatoa taswira ya mgogoro ulioenea kote nchini. Benki Kuu ya Marekani (Federal Reserve) imelazimika kudumisha viwango vya juu vya riba ili kudhibiti mfumuko wa bei, hatua ambayo imeongeza gharama za kukopa kwa kaya na wafanyabiashara. Mark Zandi, mchumi mkuu katika kampuni ya Moody’s Analytics, amekadiria kuwa jumla ya gharama ya vita vya kibiashara ni dola bilioni 220, kiasi kinacholingana na takriban dola 1,650 kwa kila kaya ya kawaida ya Marekani. Hii ni gharama ya moja kwa moja tu ambapo gharama zisizo za moja kwa moja kama vile kupungua kwa ukuaji wa uchumi, kupanda kwa mfumuko wa bei, na mashinikizo kwa wakulima na madereva wa malori ya mizigo katika eneo la Midwest, zinaongeza mzigo mkubwa kwa uchumi wa Marekani. Huku msimu wa mavuno ukikaribia, bei za dizeli na petroli zimekuwa suala muhimu katika kinyang'anyiro cha uchaguzi ujao, jambo linalouweka utawala wa Trump chini ya mashinikizo hata miongoni mwa wanachama wa chama cha Republican chenyewe. Kwa mtazamo wa kijeshi, vita vinavyohusisha Iran vimesababisha kupungua kwa akiba ya silaha za Marekani kwa kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa tena huko nyuma. Ripoti zinaonyesha kuwa jeshi la Marekani limetumia takriban asilimia 80 ya makombora yake aina ya THAAD na nusu ya makombora yake ya Patriot, huku pia likitumia karibu makombora yote ya masafa marefu ya kimkakati na yale yenye uwezo wa kulenga shabaha kwa usahihi wa hali ya juu. Hizi ndizo hasa silaha ambazo Washington inazitegemea katika kukabiliana na China katika eneo la Indo-Pasifiki na kutimiza ahadi zake za kiusalama barani Ulaya. Kujaza upya akiba hizi kunaweza kuchukua miaka mingi, ambapo tayari washirika wakuu wa Marekani wameonyesha wasiwasi kuhusu kucheleweshwa kufikishiwa silaha na kudhoofika kwa dhamana za kiusalama zinazotolewa na Washington. Kwa hivyo, vita na Iran vimepunguza pakubwa uwezo wa Marekani wa kuzuia hujuma ya adui katika nyanja nyingi, na kwa namna fulani, kuiacha Washington ikiwa katika hatari kubwa mbele ya mahasimu wake wakuu.
Katika upande wa siasa za ndani, kupungua kwa uungaji mkono wa umma kwa vita umefikia karibu asilimia 30, na hivyo kuwaweka Warepublican katika nafasi ngumu kabla ya uchaguzi wa katikati ya muhula. Seneta Jon Husted wa Republican amesema, "Vita na Iran lazima viishe haraka iwezekanavyo." Amebainisha kwamba, misimamo kama hiyo ya wagombea wengine wawili wa Seneti ya Marekani, inaashiria upinzani unaoongezeka kwa uchokozi wa utawala wa Trump dhidi ya Iran, hata miongoni mwa wanachama wa chama chake mwenyewe. Wagombea wa Republican katika majimbo muhimu sasa wanajaribu kujitenga na Trump. Hatua hii inaashiria kuwa vita dhidi ya Iran umekuwa mzigo mkubwa wa kisiasa kwa Chama cha Republican. Wapiga kura wanamtupia lawama Trump kutokana na kupanda kwa bei ya mafuta, mfumuko wa bei na mzozo unaoendelea, huku Wademocrat wakikosoa kushindwa kufikiwa malengo ya vita, na kutumia suala hilo kama silaha ya kisiasa dhidi ya chama cha Republican katika msimu huu wa uchaguzi. Hakeem Jeffries, Kiongozi wa Walio Wachache wa Chama cha Democrat katika Baraza la Wawakilishi la Marekani, awali alikosoa sera za Trump za kuchochea vita, akisema kuwa vita hivyo vya kujitakia mwenyewe vilikuwa vimeshindwa kufikia malengo yaliyotangazwa. Katika mkutano na waandishi wa habari, Jeffries amesema: "Hali ya uchumi chini ya uongozi wa Trump na chama cha Republican ni mbaya sana na inaendelea kuelekea upande usiofaa." Hivyo, hata kama vita hivi vitaisha karibuni, lakini madhara yake yataendelea kwa wiki na miezi ijayo na yanaweza kuwa sababu kuu ya kushindwa Warepublican katika Bunge la Marekani.
Jambo la msingi ni kwamba vita dhidi ya Iran sasa vinadhihirisha taratibu gharama zilizojificha za hatua za uchokozi wa kijeshi wa Marekani dhidi ya Iran. Marekani imeshindwa kabisa kufikia malengo yake makuu, kudhibiti gharama, kudumisha uwezo wake wa kijeshi, na kuimarisha imani ya washirika kwake. Kilichobakia sasa ni mchanganyiko wa mfumuko wa bei, kupungua kwa akiba za kimkakati, kutokuaminiana miongoni mwa washirika na mgogoro wa kisiasa ndani ya nchi. Kwa mtazamo huu, vita dhidi ya Iran si hata ushindi mdogo tu kwa Washington, bali ni janga la kimkakati ambalo athari zake zitaendelea kuwepo kwa muda mrefu ujao baada ya kumalizika rasmi mapigano.