Serikali ya Somalia: Mashambulizi ya kigaidi Mogadishu yamepeungua kwa 90%
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i141802-serikali_ya_somalia_mashambulizi_ya_kigaidi_mogadishu_yamepeungua_kwa_90
Waziri wa Ulinzi wa Somalia Ahmed Moallim Fiqi ametangaza kuwa, mashambulizi ya kigaidi katika mji mkuu wa nchi hiyo Mogadishu yamepungua kwa karibu asilimia 90 katika miaka ya hivi karibuni. Fiqi amesema, ripoti ya tathmini ya usalama iliyowasilishwa katika makao makuu ya Wizara ya Ulinzi katika wilaya ya Daynile jijini Mogadishu siku ya Jumamosi ilionyesha kuwa mashambulizi ya kigaidi yamepungua kwa takribani asilimia 87.
(last modified 2026-09-29T03:05:19+00:00 )
Sep 29, 2026 03:03 UTC
  • Serikali ya Somalia: Mashambulizi ya kigaidi Mogadishu yamepeungua kwa 90%

Waziri wa Ulinzi wa Somalia Ahmed Moallim Fiqi ametangaza kuwa, mashambulizi ya kigaidi katika mji mkuu wa nchi hiyo Mogadishu yamepungua kwa karibu asilimia 90 katika miaka ya hivi karibuni. Fiqi amesema, ripoti ya tathmini ya usalama iliyowasilishwa katika makao makuu ya Wizara ya Ulinzi katika wilaya ya Daynile jijini Mogadishu siku ya Jumamosi ilionyesha kuwa mashambulizi ya kigaidi yamepungua kwa takribani asilimia 87.

Ameielezea takwimu hiyo kama ushahidi wa uborekaji mkubwa wa hali ya usalama jijini humo.

"Karibu asilimia 87 ya mashambulizi ya kigaidi yamepungua, kulingana na ripoti iliyowasilishwa leo," Fiqi alisema, akiongeza kuwa serikali inalenga kuongeza kiwango hicho cha kupungua hadi zaidi ya asilimia 90 katika miezi ijayo.

Waziri huyo amelinganisha hali ya sasa na ile ya miaka kadhaa iliyopita, ambapo Mogadishu ilikumbwa mara kwa mara na mashambulizi ya silaha, ikiwa ni pamoja na miripuko na mashambulizi yaliyolenga taasisi za serikali, maeneo ya umma, na barabara kuu.

Fiqi, ameutaja uborekaji huo kuwa ni matokeo ya juhudi endelevu za idara ya intelijensia, polisi na jeshi la Somalia, pamoja na ushirikiano kutoka kwa wakazi wa eneo la Banadir, ulipo mji mkuu Mogadishu.

Waziri huyo ameongeza kuwa vikosi vya usalama pia vimepanua uwepo wao katika maeneo ambayo hapo awali hayakufikika kutokana na udhibiti wa kundi la Al-Shabaab, hatua iliyoimarisha usalama kuzunguka mji mkuu.

Fiqi amewapongeza maafisa wa usalama waliofanya kazi bila kuchoka wakati wa juhudi hizo, akisema mafanikio hayo yamepatikana kwa gharama kubwa ya maisha ya watu.

Aidha, amevisihi vikosi vya usalama na wakazi wa Mogadishu kuendelea kuwa macho, akionya dhidi ya majaribio ya kudhoofisha mafanikio ya usalama kupitia uhamasishaji wa koo au kufufua wanamgambo.
Waziri wa Ulinzi wa Somalia ametoa wito huo huku serikali ya Somalia ikilenga kuimarisha mafanikio ya usalama huko Mogadishu sambamba na kuendeleza operesheni za kijeshi dhidi ya kundi la kigaidi la Al Shabab…/