Araghchi: Tutasimama imara hata kama vita vitakuwa ni vya mwisho wa dunia
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i141788-araghchi_tutasimama_imara_hata_kama_vita_vitakuwa_ni_vya_mwisho_wa_dunia
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema kuwa: "Tulikwenda New York pamoja na mheshimiwa Rais ili kutengeneza njia ya amani; ieleweke wazi kwamba Iran itabaki imara mbele ya uchokozi wowote. Tuko tayari kwa diplomasia lakini pia tuko tayari kusimama kidete hata kwenye vita vya mwisho wa dunia."
(last modified 2026-09-28T08:01:23+00:00 )
Sep 28, 2026 08:00 UTC
  • Araghchi: Tutasimama imara hata kama vita vitakuwa ni vya mwisho wa dunia

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema kuwa: "Tulikwenda New York pamoja na mheshimiwa Rais ili kutengeneza njia ya amani; ieleweke wazi kwamba Iran itabaki imara mbele ya uchokozi wowote. Tuko tayari kwa diplomasia lakini pia tuko tayari kusimama kidete hata kwenye vita vya mwisho wa dunia."

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Mehr, Sayyid Abbas Araghchi ameandika kwenye ukurasa wake binafsi kwamba: "Katika kipindi cha *Meet the Press* cha NBC, nilisema kuwa mimi na Rais Pezeshkian hatukwenda New York kwa ajili ya vita; tulikwenda kutengeneza njia ya amani. Lakini ieleweke wazi kwamba, Iran itasimama imara dhidi ya uchokozi wowote — hata kama vitatokea vita vya mwisho wa dunia."

Vilevile Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amezungumzia mpango wa siku saba uliopendekezwa na Tehran wa kufunguliwa tena Lango-Bahari la Hormuz akisema: "Iran iko tayari kufungua tena lango-bahari hilo, lakini kwa shari kwamba Marekani ichukue hatua mahususi."

Akizungumza na kipindi cha *Meet the Press* cha televisheni ya NBC News ya Marekani Araghchi amesema: "Mpango huu unaweza kurejesha hali ya kawaida katika eneo la Ghuba ya Uajemi na Lango-Bahari la Hormuz; swali sasa ni kwa nini Marekani inakataa pendekezo hilo?"

Akielezea pendekezo hilo la siku saba la Iran kuwa liko wazi kabisa, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesema: "Tuko tayari kufungua Lango-Bahari la Hormuz, iwapo Marekani itachukua hatua mahususi. Maneno haya si mapya wala si ya kiholela; bali yanaakisi haki ambazo tunataka ziheshimiwe."

Araghchi ameendelea kusema: "Kwanza kabisa, tunataka vita vikomeshwe." Pia tunataka kuachiwa fedha na mali za Iran ambazo zimezuiliwa kinyume cha sheria, na tunataka kuweza kuuza mafuta yetu.

Waziri wa Mambo ya Nje alisisitiza kuwa mambo yaliyopendekezwa na Iran ni yale yale masuala mahususi ambayo Marekani ilikuwa imeahidi kuyatekeleza katika makubaliano ya awali. Maelezo yaliyotolewa kuhusu mpango huo wa siku saba pia yanaonesha kuwa Tehran imetaja suala la kuondolewa mashinikizo ya kijeshi na vikwazo vya mafuta pamoja na kuachiwa mali zilizozuiliwa, kama masharti ya kutekelezwa mpango huo.