Ukidhabi wa Trump washindwa kuzuia kupaa bei ya mafuta
Bei ya mafuta imeendelea kupaa katika siku ya kwanza ya wiki ya biashara, licha ya rais wa Marekani Donald Trump kueneza madai ya uongo ya kufanyika mazungumzo na Iran katika hila ya kushusha bei ya bidhaa hiyo muhimu.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Fars, bei ya mafuta duniani imevuka dola 107 kwa pipa mwanzoni mwa wiki mpya ya biashara.
Kiwango hiki kinaonyesha ongezeko la dola 2 ikilinganishwa na bei ya kufunga biashara wiki iliyopita.
Ongezeko hili limetokea licha ya Trump na mtandao wa Axios kueneza taarifa za uongo kwamba mazungumzo baina ya Marekani na Iran yameanza ili kuathiri soko la nishati duniani.
Takwimu zinaonesha kuwa, tofauti kati ya bei ya papo kwa papo (spot price) na bei ya uwasilishaji wa baadaye (mwezi mmoja ujao) imefikia kiwango cha juu kabisa, jambo linaloashiria kuweko uhaba mkubwa wa mafuta katika soko la dunia.
Siku chache zilizopita, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alisema kuwa, Marekani ndiyo inayohusika na hali iliyopo duniani leo hii; Lango-Bahari la Hormuz lilikuwa wazi kabla ya Marekani na utawala wa Kizayuni kuivamia Iran.
Rais Masoud Pezeshkian alisema hayo katika mahojiano maalumu aliyofanyiwa na televisheni ya Fox News ya Marekani na kukanusha vikali madai ya uongo kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inataka kumiliki bomu la nyuklia.
Alipoulizwa katika mahojiano maalumuu ya kipindi cha "Special Report" cha Fox News, kwamba je, mnataka bomu la nyuklia? Rais Pezeshkian alimwambia mtangazaji Bret Baier kwamba: "Hapana kabisa. Hapana kabisa. Kiongozi wetu Mkuu aliyeheshimika na kuuawa shahidi alikuwa ametangaza mara kadhaa kwamba, kwa mujibu wa fatwa na mafundisho ya Kiislamu, kitendo hiki si halali na ni kinyume na sheria."
Kuhusu makubaliano kati ya Washington na Tehran ambayo Trump alijiondoa kama alivyojiondoa pia kwenye mapatano ya nyuklia ya JCPOA, Rais Pezeshkian alisema: "Sisi Iran hatuna tatizo; tulifikia makubaliano na rais wenu. Hatukuwa tumefunga Lango la Hormuz; lango hilo lilikuwa wazi. Lakini walituvamiia na kutushambulia bila ya uhalali wowote wa kisheria. Waliwaua na kuwafanya mashahidi Kiongozi wetu Mkuu, wanasayansi wetu, makamanda wetu wa kijeshi na maafisa wa serikali yetu."
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran alisema: Tatizo ni kwamba badala ya mazungumzo, Marekani inaanzisha vita na inatuzibia njia zote. Hivi sivyo binadamu anavyopaswa kuishi. Hawawezi kutuwekea vikwazo au kuzuia uwezo wetu wa kufanya mambo.