Ufaransa: Kutoka Madai ya Haki za Binadamu hadi Ukandamizaji
https://parstoday.ir/sw/news/world-i142300-ufaransa_kutoka_madai_ya_haki_za_binadamu_hadi_ukandamizaji
Gazeti la The Guardian limeandika kuwa serikali ya Ufaransa inawachukulia wanafunzi wanaoandamana katika pembe tofauti za nchi hiyo kama "maadui wa ndani ambao lazima wadhibitiwe."
(last modified 2026-10-19T10:19:55+00:00 )
Oct 19, 2026 10:17 UTC
  • Ufaransa: Kutoka Madai ya Haki za Binadamu hadi Ukandamizaji

Gazeti la The Guardian limeandika kuwa serikali ya Ufaransa inawachukulia wanafunzi wanaoandamana katika pembe tofauti za nchi hiyo kama "maadui wa ndani ambao lazima wadhibitiwe."

Tathmini hii ya The Guardian inafichua utata mkubwa uliopo kuhusu rekodi ya serikali ya Ufaransa, inayojinadi kuwa chimbuko la haki za binadamu na mtetezi wa uhuru, ambapo sasa imeamua kutumia mbinu za ulazimishaji na ukandamizaji dhidi ya vijana wanaodai mazingira bora ya elimu na fursa sawa. Mgogoro wa sasa nchini Ufaransa hauhusu tena masuala ya elimu pekee bali umekuwa kipimo cha uhalali wa serikali ambayo, badala ya kushughulikia madai ya kizazi kipya, inawaona kama tishio kwa usalama.

Gazeti la The Guardian limefichua ukubwa wa ukandamizaji huu kwa kuelezea majeraha ya kimwili waliyopata vijana kadhaa kwenye maandamano. Eden, mwenye umri wa miaka 14, alivunjika taya na kupoteza meno baada ya kupigwa usoni na bomu la kutoa machozi. Maël, mwenye umri wa miaka 16, alipoteza uwezo wa kuona katika jicho moja, huku Evan, mwenye umri wa miaka 15, akipoteza mkono wake katika mlipuko unaohusishwa na bomu la polisi linalotumika kuzima maandamano. Haya si madhara ambayo vijana wanapaswa kuyapata kwa kudai haki yao ya elimu. Simulizi za matukio haya zinaiweka serikali ya Ufaransa mbele ya swali muhimu: Je, inawezekanaje kuzungumzia haki za binadamu huku ikipuuza uwajibikaji wake kuhusu majeraha makubwa waliyopata vijana waliokuwa kwenye maandamano ya amani?

Hasira ya wanafunzi hao inatokana na sababu iliyo wazi. Kwa mujibu wa ripoti ya The Guardian, zaidi ya saa milioni 20 za masomo hazikutolewa katika shule za sekondari za umma nchini Ufaransa katika mwaka wa masomo wa 2024–2025—kiwango ambacho ni sawa na takriban somo moja kati ya kila masomo kumi. Uhaba wa walimu, majengo ya shule yaliyochakaa, ukosefu wa vifaa vya kutosha, na ukosefu wa usawa katika elimu—hasa katika maeneo yenye changamoto—vimepunguza fursa za kielimu kwa maelfu ya wanafunzi. Wakati shule zinaposhindwa kukidhi hata mahitaji ya msingi zaidi ya elimu, maandamano ya wanafunzi hayawezi kuchukuliwa kama vurugu au tishio kwa utulivu wa umma; bali ni ishara ya kudai uwajibikaji kuhusu utendaji wa serikali.

Pamoja na hayo, badala ya kushughulikia mgogoro huo kupitia mazungumzo na mageuzi ya haraka, serikali ya Ufaransa imeamua kukabiliana na suala hilo kipolisi. Aidha, gazeti la The Guardian limeripoti kuwa, kufikia tarehe 8 Oktoba, watu 6,877 walikuwa wamekamatwa, ambapo takriban asilimia 80 kati yao walikuwa watoto au vijana walio chini ya umri wa miaka 18. Takwimu hizi, pamoja na ripoti za majeraha makubwa waliyopata vijana hao, zinaonyesha umuhimu wa kufanyika uchunguzi huru kuhusu mwenendo wa polisi. Ingawa serikali ina jukumu la kudumisha amani na utulivu wa umma, lakini mamlaka hiyo haiwezi kutumika kama kisingizio cha kutumia nguvu kupita kiasi au kupuuza haki ya kufanya maandamano.

Hapa ndipo hasa mgongano ndani ya serikali ya Ufaransa unapodhihiri wazi. Ni wazi kuwa Paris haiwezi kutumia suala la haki za binadamu kama kanuni yenye uhalali pale tu linapotajwa katika hotuba za kidiplomasia au kutumiwa kuchukua misimamo dhidi ya mataifa mengine. Kipimo halisi ni kuona namna serikali inavyoamiliana na raia wake wanapohoji sera zake wakiwa ndani ya mipaka ya nchi yao. Serikali inayowatuhumu vijana wanaoandamana wakilalamikia uhaba wa walimu na rasilimali za elimu, kama "adui wa ndani," huwa inazidi tu kupanua pengo lililopo kati yake na raia, badala ya kushughulikia matatizo yao ya msingi. Msimamo wa aina hii si tu unaharibu imani ya umma, bali pia unatilia shaka uhalali wa madai ya Ufaransa kuhusu haki za binadamu.

Maandamano kama hayo nchini Italia na Ubelgiji, pamoja na mikusanyiko ya kuonyesha mshikamano na wanafunzi hao katika mataifa mengine ya Ulaya, inaonyesha wazi kuwa hasira ya kizazi cha vijana inaweza kuvuka mipaka ya kitaifa. Ingawa baadhi ya matakwa yanaweza kutofautiana, lakini masuala ya msingi kama vile ukosefu wa rasilimali za elimu, kupanda kwa gharama za elimu, mgogoro wa nyumba, na wasiwasi kuhusu matarajio ya kiuchumi yanajumuisha nchi nyingi za Ulaya. Mfungamano huu unapasa kuwa onyo kwa serikali za Ulaya kwamba upuuzaji wa mahitaji ya kizazi kipya unaweza kubadilisha malalamiko yaliyotawanyika kuwa mgogoro mkubwa zaidi kuhusu mifumo ya kisiasa na vipaumbele vya kiuchumi.

Ufaransa inajikuta katikati ya changamoto hii. Ingawa serikali inakabiliwa na deni kubwa la umma na vikwazo vya bajeti, lakini hilo halipasi kuizuia kukosolewa. Mzozo wa sasa hauhusu tu uhaba wa rasilimali; unahusu vipaumbele vinavyotolewa na serikali na namna matumizi ya umma yanavyotengewa bajeti. Wakati shule zinakabiliwa na uhaba wa walimu na kupelekea wanafunzi kumiminika mitaani wakidai mazingira bora ya masomo, serikali ya Ufaransa inapaswa kueleza ni kwa nini hatua zinazolenga usalama zimepewa kipaumbele kuliko mageuzi katika sekta ya elimu. Serikali ya Ufaransa haiwezi kukwepa kuwajibika kuhusu muamala mbaya wa jeshi lake la polisi au hali ya shule zake kwa kujificha nyuma ya historia bandia ya eti kutetea haki za binadamu.