Rais wa Iran: Tutakabiliana na shambulio lolote kwa nguvu zote
-
Rais wa Iran: Tutakabiliana na shambulio lolote kwa nguvu zote
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, katika kipindi cha karne mbili zilizopita, Iran haijawahi kuwa nchi yenye uchokozi wala kuishambulia nchi yoyote, na haina nia ya kuishambulia nchi yoyote.
Hata hivyo, amesema Iran itakabiliana kwa nguvu na ushuujaa na shambulio lolote, hata kama itabidi kupigana hadi kutoa uhai wake, akisisitiza kuwa haitaruhusu maadui kuwa na tamaa ya kutwaa ardhi ya nchi hiyo.
Rais Masoud Pezeshkian amesema hayo leo Jumapili, wakati wa kikao cha Bunge cha kujadili na kupiga kura ya kuidhinisha uteuzi wa Mehrdad Akhlaghi waziri anayependekezwa kwa ajili ya kushifa wadhifa wa Waziri wa Ulinzi.
Katika hotuba yake, aliwakumbuka na kuwaenzi mashahidi wa thamani wa Mapinduzi ya Kiislamu, hususan mashahidi wa vita viwili vya hivi karibuni vilivyolazimishwa dhidi ya Iran, Kiongozi Shahidi wa Mapinduzi ya Kiislamu, wanafunzi waliouawa shahidi pamoja na mawaziri mashahidi wa serikali.
Pezeshkian amesema kuwa, Shahidi Meja Jenerali Aziz Nasirzadeh (waziri wa Ulinzi aliyeuawa shahidi) alikuwa mtu msomi, mnyofu, mwaminifu na aliyejitolea kwa dhati kuitumikia nchi na mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu.
Alimwomba Mwenyezi Mungu amfunike marehemu huyo kwa rehema Zake, huku akitoa salamu za heshima kwa roho za mashahidi wote wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran.
Rais wa Iran amesifu ulinzi wa kishujaa uliofanywa na vikosi vya jeshi vya taifa hili, akisema kuwa umeiwezesha Iran kupata heshima, hadhi na fahari mbele ya nchi za kigeni.
Amesisitiza kuwa dunia imeshangazwa na namna vikosi hivyo vilivyotekeleza ulinzi wa nchi na uwezo mkubwa viliouonyesha wa kustahimili mashambulizi na kusimama imara vilioonyesha.
Mwisho, amesisitiza kuwa Iran haitalegeza msimamo wake hata kidogo mbele ya tamaa, kupenda makuu na ubabe wa madola vamizi. Badala yake, amesema kuwa, taifa hili litaendelea na mshikamano, uthabiti na muqawama na katu halitasalimu amri.