Ugonjwa wa Ebola wasambaa mkoa wa nane DRC
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i142308-ugonjwa_wa_ebola_wasambaa_mkoa_wa_nane_drc
Mlipuko wa ugonjwa wa virusi vya Ebola nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) umeenea hadi katika mkoa wa nane, wakati mamlaka za afya zikijitahidi kudhibiti janga baya zaidi kuwahi kurekodiwa nchini hum.
(last modified 2026-10-19T10:31:02+00:00 )
Oct 19, 2026 10:29 UTC
  • Ugonjwa wa Ebola wasambaa mkoa wa nane DRC

Mlipuko wa ugonjwa wa virusi vya Ebola nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) umeenea hadi katika mkoa wa nane, wakati mamlaka za afya zikijitahidi kudhibiti janga baya zaidi kuwahi kurekodiwa nchini hum.

Kwa mujibu wa taarifa ya leo Jumatatu, Wizara ya Afya imesema kuwa mkoa wa Ubangi Kaskazini ulioko kaskazini-magharibi mwa Kongo umekuwa mkoa wa hivi punde kuathirika, kufuatia uthibitishwaji wa kesi mbili na kifo kimoja katika eneo linalopakana na Jamhuri ya Afrika ya Kati.

Kesi hizo mpya zinawahusisha vijana wa kiume wenye umri wa miaka 20 katika eneo la afya la Wapinda, ambalo linapakana na mkoa wa Bas-Uele.

Hadi kufikia wiki iliyopita, ugonjwa huo uliosababishwa na aina ya virusi vya Bundibugyo ulikuwa umezuiwa katika mikoa saba ambayo ni Haut-Uele, Ituri, Kivu Kaskazini, Kivu Kusini, Bas-Uele, Tshopo na Ubangi Kusini.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), maambukizi yanaendelea kuwa ya viwango tofauti katika maeneo yaliyoathirika.

Mkoa wa Ituri unasalia kuwa kitovu kikuu cha mlipuko huo, huku maambukizi makubwa yakiendelea kushuhudiwa Kivu Kaskazini na Haut-Uele.

Idadi ya kesi zilizothibitishwa za Ebola nchini Kongo imepanda na kufika zaidi ya 9,400, zikiwemo vifo 4,536 tangu kutangazwa kwa mlipuko huo mwezi Mei, kwa mujibu wa takwimu za hivi punde rasmi.

Upinzani na msimamo mkali kutoka kwa jamii unasalia kuwa miongoni mwa changamoto kubwa, huku vifo vingi vikitokea ndani ya jamii bila huduma za hospitali.

Mkurugenzi wa WHO Kanda ya Afrika, Mohamed Yakub Janabi, alisisitiza siku ya Jumapili umuhimu wa viongozi wa kijamii katika kujenga kuaminiana, umiliki wa jamii na hatua za pamoja za kukabiliana na janga hilo.

Takriban theluthi mbili ya vifo vinatokea majumbani, kwa mujibu wa takwimu za WHO.

Mlipuko huu umekuwa mkubwa na wenye maafa makubwa zaidi kuwahi kurekodiwa nchini Kongo, na wa pili kwa ukubwa duniani wa ugonjwa wa Ebola baada ya lile janga la mwaka 2014-2016 lililolikumba eneo la Afrika Magharibi.

Wakati huo huo, Wizara ya Afya ya Kenya ilithibitisha siku ya Jumapili kesi mpya moja ya ugonjwa wa Ebola, jambo ambalo linafanya idadi ya kesi zilizothibitishwa nchini humo kufikia nane mwezi huu.

Mamlaka za afya Kenya zimetoa wito wa kuongezwa kwa umakini na ulinzi mkubwa ili kuzuia kuenea zaidi kwa ugonjwa huo kuvuka mipaka ya nchi.