Deni la Marekani lavunja rekodi kutokana na vita dhidi ya Iran
https://parstoday.ir/sw/news/world-i142292-deni_la_marekani_lavunja_rekodi_kutokana_na_vita_dhidi_ya_iran
Deni la taifa la Marekani limefikia rekodi ya kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa tena, likivuka alama ya dola trilioni 40.
(last modified 2026-10-19T03:44:22+00:00 )
Oct 19, 2026 03:42 UTC
  • Deni la Marekani lavunja rekodi kutokana na vita dhidi ya Iran
    Deni la Marekani lavunja rekodi kutokana na vita dhidi ya Iran

Deni la taifa la Marekani limefikia rekodi ya kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa tena, likivuka alama ya dola trilioni 40.

Deni la taifa la Marekani hivi karibuni limevuka mstari wa dola trilioni 40, kiasi kwamba ni vigumu kuelewa ukubwa wake halisi. Wakati Donald Trump alipoapishwa kwa muhula wake wa pili wa urais mwezi Januari 2025, deni la Marekani lilikuwa dola trilioni 36.2. Ongezeko la karibu dola trilioni 4 ndani ya kipindi kifupi kama hiki linaashiria hali isiyo na mfano wake ya serikali kukopa fedha.

Mhanga wa kwanza wa mwelekeo huu ni bajeti ya serikali ya Marekani. Kwa sasa, serikali inatumia fedha nyingi zaidi kulipa riba ya madeni ya zamani kuliko inavyotumia kwa ajili ya ulinzi wa taifa au kutoa huduma za afya kwa mamilioni ya raia. Mfumo wa kifedha wa Washington umebadilika kiasi kwamba sehemu inayozidi kuongezeka ya rasilimali za umma inaelekezwa kwa wenye hati fungani, huku madeni ya zamani yakimeza bajeti iliyokusudiwa kutoa huduma kwa vizazi vijavyo.

Wakati raia wa Marekani wanakabiliwa na takwimu hizi za kutisha, ripoti zinaonyesha kuwa utajiri binafsi wa Donald Trump umeongezeka kwa takriban dola bilioni 2.2 wakati wa muhula wake wa pili wa urais.

Wanawe wakubwa, Eric na Donald Trump Jr., nao wamejiunga na makampuni ya uwekezaji, ambapo inaripotiwa kuwa mwanawe wa miaka 20, Barron Trump, amekusanya utajiri wa dola milioni 150 kupitia sarafu za kidijitali. Mrundiko wa utajiri binafsi na wa familia ya rais wa Marekani, unaoenda sambamba na ongezeko la deni la taifa, unazua maswali mengi kuhusu vipaumbele vya kiuchumi vya utawala huo.

Wanasiasa wa vyama vyote viwili vikuu wamechangia katika ukuaji wa deni la Marekani kwa miongo kadhaa; hata hivyo, kasi ya sasa ya ongezeko hilo haijawahi kushuhudiwa tena huko nyuma. Aidha, gharama za kijeshi zinaendelea kuongezeka bila kusimama.  Vita vya muda mrefu dhidi ya Iran vimeigharimu hazina ya serikali makumi ya mabilioni ya dola moja kwa moja, wakati ambao mamilioni ya kaya za Marekani zinatatizika katika kulipa bili zao za kila mwezi na kukidhi mahitaji yao ya msingi.

Deni linaloongezeka la serikali lina matokeo ambayo yanaenea zaidi ya takwimu za uhasibu tu. Ili kufidia malipo ya riba ya deni hili, serikali inalazimika kupunguza huduma za ndani au kufadhili majukumu yake kwa kuongeza usambazaji wa pesa. Kupunguzwa kwa bajeti kunaweza kudhoofisha mfumo wa afya ya umma, miundombinu ya usafiri, mashirika ya misaada, na utafiti wa kimatibabu.