Bunge lamuidhinisha Mehrdad Akhlaghi kuwa Waziri mpya wa Ulinzi wa Iran
Bunge la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran limemuidhinisha Mehrdad Akhlaghi kuwa Waziri mpya wa Ulinzi wa majeshi ya Iran, huku wabunge wakipiga kura kwa wingi kupitisha uteuzi wake.
Bunge lilipitia sifa na mipango ya Akhlaghi katika kikao chake cha Jumapili, kilichoongozwa na Spika Mohammad Baqer Qalibaf, kabla ya kupiga kura ya kumteua. Akhlaghi alipata kura 237 za ndio na 15 za hapana, huku kukiwa hakuna kura ambayo haikupigwa, kati ya kura zote 277 zilizopigwa, na hivyo kumfanya kuwa waziri mpya wa ulinzi.
Rais Masoud Pezeshkian alimteua Akhlaghi kushikilia wadhifa huo mnamo tarehe 5 Oktoba, na kuwasilisha jina lake pamoja na historia yake ya kitaaluma bungeni ili kuidhinishwa rasmi.
Katika kikao cha Jumapili, wabunge walisikiliza ripoti kutoka kwa kamati za bunge zinazohusika na usalama wa taifa na sera za kigeni, pamoja na ile ya viwanda na madini, ambazo zilikuwa zimechunguza mipango iliyopendekezwa na Akhlaghi.
Pezeshkian pia alizungumza bungeni kwa ajili ya kumtetea waziri huyo, huku wabunge waliopinga na wale waliounga mkono mipango yake wakiwasilisha maoni yao, kabla ya Akhlaghi kupewa fursa ya kutetea mipango aliyopendekeza.
Wiki iliyopita, Akhlaghi alifanya mikutano miwili na wabunge katika kufafanua mipango yake na kusikiliza maoni yao. Vilevile alikutana na makamanda wa Jeshi la Iran pamoja na wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) ili kufahamu vipaumbele vyao.
Akhlaghi anachukua nafasi ya Aziz Nasirzadeh, ambaye aliuawa shahidi katika mashambulizi ya kigaidi yaliyofanywa na Marekani pamoja na Israel dhidi ya Tehran mwanzoni mwa uchokozi wa vita vya siku 40. Kufuatia tukio hilo, Pezeshkian alimteua Brigedia Jenerali Seyyed Majid Ibn al-Reza kuwa kaimu waziri wa ulinzi.
Katika maelezo yake bungeni kabla ya kupigiwa kura, Akhlaghi alisisitiza kuwa Iran itatoa jibu kali iwapo maadui zake wataanzisha shambulio jipya dhidi ya nchi hii.
"Ikiwa adui Mmarekani-MZayuni atafanya makosa mengine ya kimahesabu, jibu la taifa la Iran na wapiganaji wa Kiislamu litakuwa la kushangaza na kubwa mno," amesema.
Akhlaghi pia ameonya kuwa Washington na washirika wake watabeba dhima ya matokeo ya kikanda na kimataifa ya uchokozi wowote mpya dhidi ya Iran.
Ameongeza kuwa, nguvu ya ulinzi ya Iran haitegemei tu uwezo wake wa kioperesheni uwanjani, bali pia uelewa wake wa mazingira ya kimkakati.