Rais Pezeshkian: Trump anaota ndoto za kuiangamiza Iran
-
Rais Pezeshkian: Trump anaota ndoto za kuiangamiza Iran
Rais Masoud Pezeshkian wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, “Rais wa Marekani anaota ndoto za kuifuta, kuiangamiza na kuipindua Iran, kwa sababu taifa letu linafanya juhudi kwa nguvu na uthabiti, na litaweza kushinda vikwazo vyote.”
Kwa mujibu wa Ofisi ya Rais wa Iran, Rais Masoud Pezeshkian amesema hayo leo Jumapili, iliyosaidifiana na kuanza Wiki ya Utalii ambapo amezindua kwa njia ya mtandao miradi 246 ya Wizara ya Urithi wa Utamaduni, Utalii na Kazi za Mikono.
Rais wa Iran ameisisitiza umuhimu wa kupanua kiwango cha mahusiano ya kiutamaduni na utalii na nchi jirani. Amesema kutokana na vikwazo ambavyo Marekani imeiwekea Iran, ni muhimu kuendeleza uhusiano wa kiutamaduni, utalii na kibiashara na nchi jirani, jambo ambalo litasaidia kuiweka nchi katika njia ya maendeleo na ustawi.
Rais wa Iran, akiashiria ushiriki wake katika Mkutano wa 81 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na hatua zilizochukuliwa wakati wa ziara hiyo, alisema:
“Yaliyofikiwa katika Umoja wa Mataifa yalijengwa juu ya msingi wa historia, utamaduni na ustaarabu wa watu mashuhuri wa Iran; watu ambao, licha ya kukabiliwa na matatizo, wameendelea kuunga mkono mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu kwa uwepo wao wa kudumu. Hata wale ambao hawakuwepo uwanjani, kwa mshikamano na ushirikiano wao, wametufanya tujivunie kuwa watumishi wao.”
Rais Pezeshkian akiendelea kukosoa kauli za Trump kuhusu tishio la kuiangamiza Iran, alisema:
“Katika nchi kubwa ya Iran kuna zaidi ya vitu milioni moja vya kihistoria, ambapo 43,000 kati yake vimesajiliwa rasmi. Marekani ina vitu vingapi vya kihistoria ambavyo vimesajiliwa kama ilivyo kwa ustaarabu wa Iran na kuwa sehemu ya urithi wake wa kihistoria?”
Dakta Pezeshkian amesema: Kwa Rais wa Marekani, haki za binadamu, sheria za kimataifa na kanuni za kibinadamu ni mambo yasiyo na msingi, kwa sababu anawatishia watu wa Iran kuwaangamiza. Hata hivyo, wananchi wenye nguvu na hadhi wa Iran watatoka katika matatizo na vikwazo kwa fahari, na watashiriki katika uzalishaji na ujenzi wa nchi yao.
Rais wa Iran, akiwapongeza wananchi kwa umoja na mshikamano wao dhidi ya maadui, amesema: Marekani na Israel, ambao ni wahalifu, hawakuamini kwamba wananchi wa Iran wangeweza kubaki imara licha ya kuwepo changamoto mbalimbali nchini. Walidhani kwamba nchi hii ingeanguka na kusambaratika kutoka ndani.