Idadi ya Wapalestina waliouawa shahidi Ghaza imepindukia 74,000
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i141804-idadi_ya_wapalestina_waliouawa_shahidi_ghaza_imepindukia_74_000
Wizara ya Afya ya Palestina katika Ukanda wa Ghaza imetangaza kuwa, idadi ya Wapalestina waliouawa shahidi tangu utawala wa kizayuni wa Israel ulipoanzisha vya kinyama dhidi ya eneo hilo mnamo Oktoba 7, 2023, imefikia 74,022 na idadi ya majeruhi imefikia 175,098.
(last modified 2026-09-29T03:10:14+00:00 )
Sep 29, 2026 03:07 UTC
  • Idadi ya Wapalestina waliouawa shahidi Ghaza imepindukia 74,000

Wizara ya Afya ya Palestina katika Ukanda wa Ghaza imetangaza kuwa, idadi ya Wapalestina waliouawa shahidi tangu utawala wa kizayuni wa Israel ulipoanzisha vya kinyama dhidi ya eneo hilo mnamo Oktoba 7, 2023, imefikia 74,022 na idadi ya majeruhi imefikia 175,098.

Kwa mujibu wa taarifa ya wizara hiyo, katika kipindi cha saa 24 zilizopita, Wapalestina wengine wanne wameuawa shahidi katika ukanda huo uliowekewa mzingiro, na wengine 19 wamejeruhiwa.

Wizara ya Afya ya Palestina huko Ghaza imeeleza pia kwamba, tangu yalipotangazwa makubaliano ya usitishaji mapigano mnamo mwezi Oktoba mwaka jana, hadi sasa Wapalestina 1,421 wameuawa shahidi na wengine 4,983 wamejeruhiwa kutokana na mashambulio yanayoendelea kufanywa na jeshi la utawala wa kizayuni.

Wakati huo huo, mwandishi wa habari wa Kituo cha Habari cha Palestina huko Ghaza ameripoti kuwa, Mpalestina mmoja amejeruhiwa kufuatia ufyatuaji risasi wa jeshi la utawala ghasibu wa Israel huko Jabalia al-Balad kaskazini mwa Ukanda wa Ghaza.

Katika tukio jengine, magari ya kijeshi ya utawala wa kizayuni yameizingira Hospitali ya Kamal Adwan kaskazini mwa Ghaza, na kupelekea wafanyakazi wa kitengo cha tiba cha hospitali kulihama jengo la hospitali hiyo kama hatua ya tahadhari hadi hali hiyo ya hatari itakapotoweka.

Katika upande mwingine, ndege za kivita za Israel zimefanya mashambulizi mawili ya anga kuzunguka Mtaa wa Al-Nafq mashariki mwa Jiji la Ghaza.

Katika mashambulizi hayo, ndege hizo za kivita za jeshi la kizayuni zimelenga paa la nyumba moja katika eneo la Al-Mashahra kwenye Mtaa wa Al-Nafq mashariki mwa Jiji la Ghaza, na kuwajeruhi Wapalestina kadhaa.

Nyumba hiyo ilikuwa makazi ya watu waliolazimika kuyahama makazi yao.

Shambulio hilo limepelekea kujeruhiwa Wapalestina kadhaa, ambapo hali za baadhi yao zimeripotiwa kuwa mahututi…/