Ethiopia yazituhumu Eritrea, Sudan na Misri kwamba, zinawaunga mkono wanamgambo wa Tigray
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i141838-ethiopia_yazituhumu_eritrea_sudan_na_misri_kwamba_zinawaunga_mkono_wanamgambo_wa_tigray
Ethiopia imezituhumu Eritrea, Sudan na Misri kuwa zinawaunga mkono wanamgambo wa Tigray, hatua ambayo Addis Ababa inaiona kuwa tishio kwa usalama na utulivu wa nchi.
(last modified 2026-09-30T12:14:28+00:00 )
Sep 30, 2026 11:46 UTC
  • Ethiopia yazituhumu Eritrea, Sudan na Misri kwamba, zinawaunga mkono wanamgambo wa Tigray
    Ethiopia yazituhumu Eritrea, Sudan na Misri kwamba, zinawaunga mkono wanamgambo wa Tigray

Ethiopia imezituhumu Eritrea, Sudan na Misri kuwa zinawaunga mkono wanamgambo wa Tigray, hatua ambayo Addis Ababa inaiona kuwa tishio kwa usalama na utulivu wa nchi.

Tuhuma hizo zinaibua tena mvutano wa kikanda katika Pembe ya Afrika, ambako uhusiano kati ya Ethiopia na majirani zake umekuwa na changamoto mbalimbali.

Jeshi la Ethiopia linazishutumu Eritrea, Sudan, na Misri kwa kuhusika kwa kiasi fulani na hali hiyo.

Mkuu wa jeshi wa Ethiopia amesema kwamba nchi hizo tatu zinawaunga mkono waasi wa Tigray. Hata hivyo Eritrea na Sudan zimetoa taarifa zikipinga madai hayo na kuyataja kuwa, hayana msingi wowote.

Pamoja na hayo, wajuzi wa mambo wanasema kuwa Eritrea imeanza kusogea karibu na kujenga uhusiano na mamlaka za waasi wa Tigray ". Inaonekana kwamba Eritrea inatumiwa kama ngome ya nyuma na majeshi ya Tigray ya TPLF na kwamba, maafisa wa Eritrea wapo huko Tigray".

Mapigano hayo yameenea kutoka eneo la Tigray hadi maeneo jirani ya Afar na Amhara, baada ya makundi saba yenye silaha kutangaza kuunda muungano unaoitwa Ethiopian Peoples’ Forces Alliance for Survival, wenye lengo la kuiondoa madarakani serikali ya Waziri Mkuu Abiy Ahmed.

Katika eneo la Afar, mapigano ya hivi karibuni yamejikita katika maeneo yanayozunguka Abala, ambako jeshi limekuwa likijaribu kuzuia waasi kutwaa udhibiti wa eneo hilo.

Hayo yanajiri katika hali ambayo, Volker Türk Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, ameonya kuhusu athari za ongezeko la mapigano nchini Ethiopia.

Matukio ya hivi karibuni yamezua hofu ya uwezekano wa kurejea mgogoro wa umwagaji wa damu, hasa ikizingatiwa kwamba vita vya miaka miwili kati ya wanajeshi wa serikali ya shirikisho la Ethiopia na wapiganaji TPLF vilivyoanza tangu mwezi Novemba 2020 hadi Novemba 2022 vilisababisha vifo vingi mbali na wimbi la wakimbizi na uharibifu wa mali.