Botswana yaadhimisha miaka 60 ya uhuru
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i141860-botswana_yaadhimisha_miaka_60_ya_uhuru
Botswana imeadhimisha miaka 60 ya uhuru kupitia sherehe za kitaifa zilizojumuisha maonyesho ya kitamaduni na shughuli mbalimbali za kusherehekea, zikiakisi miongo sita ya ustahimilivu na ustawi wa taifa hilo la kusini mwa Afrika.
(last modified 2026-10-01T12:24:16+00:00 )
Oct 01, 2026 12:21 UTC
  • Botswana yaadhimisha miaka 60 ya uhuru
    Botswana yaadhimisha miaka 60 ya uhuru

Botswana imeadhimisha miaka 60 ya uhuru kupitia sherehe za kitaifa zilizojumuisha maonyesho ya kitamaduni na shughuli mbalimbali za kusherehekea, zikiakisi miongo sita ya ustahimilivu na ustawi wa taifa hilo la kusini mwa Afrika.

Rais Duma Boko wa Botswana na mwenzake wa Msumbiji, Daniel Chapo ambaye alikuwa katika ziara rasmi nchini humo walihudhuria sherehe hizo za maadhimisho ya miaka 60 zilizofanyika Gaborone, mji mkuu wa Botswana, chini ya kaulimbiu inayosema: "Kujenga Ustahimilivu, Kuchochea Ustawi."

Maandamano ya kuvutia katika mitaa ya Main Mall kitovu cha shughuli za kijamii na kibiashara jijini humo yalionesha utamaduni wa asili wa Botswana, vikundi vya ngoma vya kuvutia sambamba na gwaride la kijeshi, huku maelfu ya wananchi wakipeperusha bendera ya taifa.

Hafla hiyo iliangazia utambulisho wa Botswana kupitia sanaa ya ufumaji wa vikapu vya asili, eneo la Delta ya Okavango, wanyamapori, mifugo, mtama, almasi, kazi za mikono za kitamaduni na nembo za taifa.

Katika ujumbe wake wa uhuru, Rais Boko ameielezea miaka 60 ya kujitawala Botswana kuwa ni tukio muhimu sana katika historia ya taifa hilo, ambalo lilipata uhuru wake tarehe 30 Septemba 1966.

"Ni wakati wa kutafakari safari ya ajabu tuliyopitia kama taifa, kusherehekea mafanikio ya nchi yetu tunayoipenda, kuwaenzi wale waliochangia katika maendeleo yake, na kuhuisha ahadi yetu ya kuzingatia maadili ambayo yameiongoza Botswana tangu kupata uhuru," amesema Rais Boko.

Vilevile amewataka wananchi kudumisha umoja licha ya tofauti zao, kuwa imara na wastahimilivu katika kukabiliana na changamoto na kujitolea kujenga Botswana yenye amani, ustawi na inayojumuisha watu wote.

Masoko ya kazi za mikono, maonyesho ya vyakula vya kitamaduni asili na matamasha ya muziki pia yamefanyika katika wilaya mbalimbali nchini humo.

Jumanne jioni pia, sherehe nyingine zilifanyika katika Uwanja wa Taifa jijini Gaborone, zikionesha ubunifu, vipaji na maonyesho mbalimbali ya kitamaduni ya Botswana na kuhitimishwa kwa onyesho kubwa la fataki.