Polisi Afrika Kusini wakabiliana kwa nguvu kubwa na uchimbaji haramu wa madini
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i141844-polisi_afrika_kusini_wakabiliana_kwa_nguvu_kubwa_na_uchimbaji_haramu_wa_madini
Polisi nchini Afrika Kusini wamewatia mbaroni zaidi ya washukiwa 100 wanaohusishwa na vikundi haramu vya uchimbaji madini ambavyo pia vinahusishwa na ufyatuaji risasi katika mikahawa, hivi karibuni, katika jimbo la Gauteng.
(last modified 2026-10-01T02:51:22+00:00 )
Oct 01, 2026 02:44 UTC
  • Polisi Afrika Kusini wakabiliana kwa nguvu kubwa na uchimbaji haramu wa madini

Polisi nchini Afrika Kusini wamewatia mbaroni zaidi ya washukiwa 100 wanaohusishwa na vikundi haramu vya uchimbaji madini ambavyo pia vinahusishwa na ufyatuaji risasi katika mikahawa, hivi karibuni, katika jimbo la Gauteng.

Operesheni kubwa ya usalama imeimarisha uchunguzi wa vitendo vinavyoendelea vya vurugu, upatikanaji wa silaha nzito na vitendo vya uhalifu vinavyofanywa na magenge yenye mitandao mipana haramu ya uchimbaji madini yaliyoenea kila mahali nchini humo.

 

Operesheni ya kutiwa mbaroni watu hao ilianza baada ya kutokea shambulio la mauaji Jumamosi usiku huko Wedela, mji ulioko karibu na kitovu cha uchimbaji dhahabu cha Carletonville, yapata kilomita 80 kusini magharibi mwa Johannesburg. Watu kumi na nane waliuawa baada ya watu wenye silaha nzito kuvamia mkahawa mmoja wa eneo hilo karibu saa 3:30 usiku na kuwafyatulia risasi ovyo watu waliokuwemo kwenye mkahawa huo.

 

Polisi wana wasiwasi kwamba tukio hilo lilikuwa ni shambulio la kulipiza kisasi lililohusishwa na ugomvi wa kimaeneo kati ya vikundi haramu vya uchimbaji madini, kwa sababu mwezi uliopita pia kulikuwa na ufyatuaji risasi kama huo katika mkahawa huo huo.

 

Katika kukabiliana na tishio hilo, polisi wa Gauteng walitangaza Jumanne kwamba vikosi vya usalama vya mashirika mengi viliwatia mbaroni watu 121 wanaotuhumiwa kuendesha operesheni haramu za kuchimba madini kinyume cha sheria. Polisi hao walikamata pia silaha tano, ikiwa ni pamoja na bunduki ya AK-47 na bunduki tatu za mkononi, pamoja na mitungi ya gesi na vifaa maalumu vya uchimbaji madini wakati wa msako wa pamoja uliopewa jina la "Operesheni Prosper."

 

Brigeri Brenda Muridili, msemaji wa Jeshi la Polisi la Afrika Kusini huko Gauteng, amesema kwamba, tangu mwezi Machi, kikosi kazi cha pamoja kinachojumuisha polisi, timu maalumu za kukabiliana na uhalifu kimkakati na Jeshi la Ulinzi wa Taifa la Afrika Kusini kimetumwa kwenda kulinda usalama katika wilaya zenye hatari kubwa kutokana na shughuli nyingine za uchimbaji madini.