Rais Pezeshkian: Tumeazimia kuvishinda vita vya kiuchumi pia vya adui
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i142046-rais_pezeshkian_tumeazimia_kuvishinda_vita_vya_kiuchumi_pia_vya_adui
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza katika mkutano na makamanda wa vikosi vya jeshi la polisi kote nchini: "tumeazimia na tumejitolea kuwatumikia wananchi kwa moyo wetu wote na kuvishinda pia vita vya kiuchumi vya adui".
(last modified 2026-10-08T11:57:51+00:00 )
Oct 08, 2026 11:55 UTC
  • Rais Pezeshkian: Tumeazimia kuvishinda vita vya kiuchumi pia vya adui

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza katika mkutano na makamanda wa vikosi vya jeshi la polisi kote nchini: "tumeazimia na tumejitolea kuwatumikia wananchi kwa moyo wetu wote na kuvishinda pia vita vya kiuchumi vya adui".

Katika mkutano huo uliofanyika mapema leo, Rais Masoud Pezeshkian ameienzi roho toharifu ya Jemadari Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu Imam Khomeini (MA), Kiongozi Shahidi wa Mapinduzi Ayatullah Khamenei, na Mashahidi wote wa njia ya kusimamia amani na uhuru wa nchi, hususan Mashahidi wa jeshi la polisi na akasema: "tumehudhuria hadhara hii kwa kuthamini mapambano na juhudi zenu za usiku na mchana katika kulinda usalama wa nchi".

Pezeshkian ameashiria jaribio la adui la kuzusha machafuko baada ya shambulio la kijeshi nchini, na akawahutubu makamanda wa jeshi la polisi akisema: "adui alikuwa akijaribu kuitumbukiza nchi kwenye machafuko baada ya shambulio la kijeshi, lakini kwa juhudi zenu za kutwa kucha mliilinda ardhi ya nchi, mkaizima njama ya adui na kumkatisha tamaa; juhudi zenu kubwa zinastahili sifa na pongezi".

Rais Pezshkian amesema, adui alidhani kwamba kwa kumuua shahidi Kiongozi Mkuu na makamanda na kuvilenga vituo vya usalama na vya jeshi la polisi, ataweza kufikia malengo yake ya kuzusha machafuko ya ndani, na akaongeza kwamba: "wao walishambulia, lakini nyinyi mlisimama imara, na wananchi nao walijitokeza uwanjani kwa ilhamu ya Mwenyezi Mungu, na Iran ikabaki na heshima".

Akizungumzia ziara yake ya kutembelea majengo ya jeshi la polisi yaliyoharibiwa wakati wa vita vya hivi karibuni, Dokta Pezeshkian amesema, mashambulizi hayo ni kielelezo dhahiri cha dhati ya kinyama na kishenzi ya Marekani na utawala wa Kizayuni, na akaongeza kwamba: "wale wanaojigamba kuwa watetezi wa haki za binadamu, katika matendo yao hawajali chochote isipokuwa ubabe na utumiaji mabavu."

Rais Pezeshkian ameashiria mabadiliko ya mtazamo yaliyotokea katika nchi nyingi duniani kuhusiana na Iran baada ya matukio ya hivi karibuni, na akasema: "leo, viongozi wa nchi nyingi wanaokutana nasi wanaitazama Iran kwa mtazamo tofauti, na hakuna nchi yoyote katika eneo iliyodhani kama Iran itaweza kuhimili mashambulizi ya kinyama kama hayo".

Akizungumzia vita vikali vya kiuchumi vya adui dhidi ya nchi, Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema: "wametumia kila shinikizo na vikwazo walivyoweza dhidi yetu ili tusiweze kuwatumikia watu wetu, lakini tumeazimia kuwatumikia wananchi kwa nguvu zetu zote na kukidhi mahitaji yao. Mradi tu tuna wananchi, hatuogopi hatari wala adui yeyote, na wananchi nao inapasa wajue kwamba sisi hatukuja kwenye uongozi kwa ajili ya kutawala, bali kutumikia wananchi"…/