Chanjo mpya ya Ebola yaanza kufanyiwa majaribio nchini Uganda
-
Chanjo mpya ya Ebola yaanza kufanyiwa majaribio nchini Uganda (USUBUHI)
Chanjo inayotarajiwa kutumika kupambana na virusi vya ugonjwa habari wa Ebola aina ya Bundibugyo imeingia katika hatua mpya ya majaribio ya kitabibu nchini Uganda, huku juhudi zikiongezeka za kuzalisha chanjo za virusi hivyo ndani ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Wessam Mankoula, afisa wa "Africa CDC" amewaambia waandishi wa habari kwa njia ya Intaneti kwamba majaribio ya Awamu ya Ib ya chanjo ya ChAdOx1 BDBV yalianza nchini Uganda tarehe 6 Oktoba, baada ya kuanza majaribio ya Awamu ya Ia nchini Uingereza mwezi Julai mwaka huu.
Vilevile amesema: "Chanjo nyingine iliyotengenezwa na kampuni ya Moderna, ilipata kibali cha kimaadili kwa ajili ya majaribio ya Awamu ya Ib nchini Uganda tarehe 7 Oktoba, baada ya majaribio yake ya Awamu ya Ia kuanza nchini Canada mwanzoni mwa mwezi Agosti."
Mripuko unaoendelea hivi sasa wa ugonjwa huo umesababishwa na virusi vya Ebola aina ya Bundibugyo ambavyo kwa sasa havina chanjo wala matibabu yoyote yaliyoidhinishwa mahususi kwa ajili yake.
Wakati huo huo, "Africa CDC" imesema kuwa DRC imepokea dozi 70,000 za chanjo ya Ervebo ambayo imeidhinishwa kutumika kupambana na virusi vya Ebola aina ya Zaire lakini haijathibitishwa kuwa na ufanisi wa kupambana na virusi aina ya Bundibugyo.
Chini ya mpango unaozingatia itifaki maalumu ya matumizi na kufikia tarehe 7 Oktoba, wafanyakazi wa afya na wengine walioko mstari wa mbele 7,775 walikuwa wameshapigwa chanjo. Wafanyakazi wengine 848 walioko mstari wa mbele walikuwa wamepokea chanjo hiyo chini ya itifaki tofauti ya utafiti inayojulikana kwa jina la BRAVO.
Kwa mujibu wa takwimu za hivi karibuni zilizotolewa na mamlaka za afya za DRC, hadi tarehe 6 mwezi huu wa Oktoba, mripuko huo ulikuwa umerekodi kesi 8,728 zilizothibitishwa za ugonjwa huo wa Ebola Bundibugyo na vifo 4,205, huku kiwango cha vifo kutokana na ugonjwa huo kikiwa ni asilimia 48.2. Jumla ya wagonjwa 2,269 walikuwa wamepona.