Jenerali Talaei-Nik: Uzalishaji silaha Iran si tu haujapungua, bali umeongezeka maradufu
-
Jenerali Talaei-Nik, msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya Iran
Msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya Iran amesema kuwa, uzalishaji wa silaha za kimkakati katika maeneo salama ndani ya Iran umehakikisha kuwa uwezo wa ulinzi wa Janmhuri ya Kiislamu unabaki salama, imara na mkubwa zaidi ambao hauathiriwi na mashambulizi ya adui.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Mehr, Jenerali Reza Talaei-Nik amesema hayo katika kipindi maalumu cha habari na kuongeza kuwa, mfumo wa kiulinzi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran umebuniwa kwa namna ambayo, changamoto mbalimbali zikiwemo za mashambulizi ya maadui, hazipelekei kusita hata mara moja uzalishaji silaha kwenye maeneo salama na kujiimarisha kijeshi.
Msemaji huyo wa Wizara ya Ulinzi ya Iran aidha amesema: Mazingira ya vita yalihitaji kuwa na Waziri wa Ulinzi mwenye sifa kama zile za marehemu Nasirzadeh au Shamkhani ambao waliweka misingi ya kujengwa viwanda vingi vya kimkakati miongo kadhaa iliyopita. Kwa mfano Kamanda Shamkhani alianzisha hatua muhimu katika sekta ya makombora na maeneo mengine wakati wa kipindi chake cha uongozi miaka 27 au 28 iliyopita, njia ambayo iliendelezwa baadaye na mawaziri waliofuata.
Amesisitiza kuwa mbinu hiyo inaendana na mahitaji ya vita pamoja na vipaumbele vya sekta ya ulinzi na vifaa vya kijeshi nchini Iran.
Brigedia Jenerali Talaei-Nik ameongeza kuwa: "Tunatumai kwamba uteuzi wa waziri mpya wa ulinzi wa Iran, kwa kuzingatia uzoefu wake mkubwa na utumishi wake katika sekta mbalimbali, ikiwa ni pamoja na nafasi yake ya hivi sasa kama mkuu wa Shirika la Viwanda vya Ulinzi na muda mrefu amekuwa akiongoza Shirika la Anga la Wizara ya Ulinzi, utaharakisha na kuboresha zaidi sekta ya ulinzi ya Iran.
Katika sehemu nyingine ya mahojiano hayo, Msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya Iran ametoa sifa nyingine za mtu aliyeteuliwa kushika nafasi ya Waziri wa Ulinzi wa Iran akisema: "Mhandisi Akhlaghi amekuwa meneja na mtaalamu muhimu katika maendeleo ya makombora aina ya Emad, Haj Qasem na Sejjil. Amekuwa na jukumu muhimu katika kuongeza uwezo wa uzalishaji na kutumia ipasavyo utaalamu wa wasomi na makampuni ambayo msingi wake ni elimu na maarifa nchini Iran."