Watu 71 wauawa katika mapigano ya kijamii huko Rumbek, Sudan Kusini
Serikali ya Sudan Kusini imetangaza kuwa, takriban watu 71, wakiwemo wanajeshi wameuawa katika mapigano ya kijamii kwenye Jimbo la Lakes la nchi hiyo.
Wizara ya Habari, Mawasiliano, Teknolojia na Huduma za Posta ya Sudan Kusini imetangaza habari hiyo na kuongeza kuwa, idadi ya vifo vilivyotokana na mapigano hayo ya jana Ijumaa, yaliyoanza katika mji wa Rumbek kati ya jamii hasimu, inatarajiwa kuongezeka kwani habari za ndani za mapigano hayo na hasara zake bado hazijapatikana.
Katika taarifa yake iliyotolewa huko Juba, mji mkuu wa Sudan Kusini, wizara hiyo ya imesema: "Kwa mujibu wa ripoti za awali, takriban watu 71 wameuawa, ingawa idadi kamili ya waliouawa na waliojeruhiwa bado haijathibitishwa na kuna uwezekano mkubwa idadi ikawa kubwa zaidi ya hiyo ya watu 71."
Taarifa hiyo imeongeza kuwa wanajeshi wanne, akiwemo kapteni na maafisa watatu wasio na vyeo vya juu kwa kifupi NCOs, wameuawa, na kwamba vikosi vya pamoja vya usalama vinavyojumuisha jeshi, polisi na idara ya ujasusi vimetumwa kurejesha utulivu huko Rumbek.
"Mji wa Rumbek kwa sasa uko chini ya udhibiti wa vikosi vya usalama vya serikali, na juhudi zinaendelea kurejesha hali ya kawaida na kuimarisha usalama na ulinzi wa raia na mali zao," imesema taarifa Wizara ya Habari, Mawasiliano, Teknolojia na Huduma za Posta ya Sudan Kusini.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa, baadhi ya raia wenye silaha waliohusika katika mapigano hayo wamekamatwa kama ambavyo vikosi vya serikali vya kulinda usalama wa raia vimekamata pia silaha zinazoaminika kuwa ndizo zilizotumika katika mauaji na mapigano hayo.
Sudan Kusini ina migogoro mingi ambayo haijulikani itatatuliwa lini. Miongoni mwa migogoro yake mikubwa na mapigano ya mara kwa mara baina ya makundi na jamii tofauti hasimu kwenye nchi hiyo changa zaidi barani Afrika.