Rwanda: Amani Maziwa Makuu inahitaji kushughulikia tishio la FDLR
-
Justin Nsengiyumva, Waziri Mkuu wa Rwanda
Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na Rwanda, zimelaumiana kuhusu utekelezwaji wa mikataba ya kumaliza vita katika eneo la Maziwa Makuu.
Lawama hizo za pande mbili zimetolewa katika hotuba za wawakilishi wa nchi hizo, katika Mkutano wa 81 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, unaoendelea mjini New York Marekani.
Waziri Mkuu wa Rwanda Justin Nsengiyumva amesema kuwa nchi yake inamaamini kuwa amani ya kudumu katika eneo la Maziwa Makuu inaweza kupatikana tu, iwapo sababu kuu za mzozo huo likiwemo kundi la waasi wa FDLR litaangaziwa.
“Rwanda inatoa wito kwa wadau wote, likiwemo Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa, kuunga mkono jitihada za kupata amani, na kuhimiza pande zote kutekeleza makubaliano yote. Hakuna suluhu ya kudumu bila ya kushughulikia, chanzo cha tatizo hili la usalama na kushughulikia malalamiko ya watu wote walioathiriwa.” Ameeleza Justin Nsengiyumva.
Kwa upande wake Judith Suminwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo amesema kuwa, Kinshasa inatambua jitihada za jamii ya kimataifa kusaidia kupata amani ya kudumu, lakini inataka kuheshimiwa mikataba iliyosainiwa.
“Hatua ya tarehe nane Septemba ambapo kwa msaada wa Kikosi cha Kulinda Amani cha Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya congo (MONUSCO) ya kuwarudisha watu 120 wanaohusishwa na kundi la FDLR, kundi ambalo kwa miaka mingi limeendelea kuweko mashariki mwa DRC, kama ilivyotakiwa na Rwanda, ni hatua muhimu na hakuna sababu kwamba uwepo wao nchini mwetu ni kisingizio cha hali inayoendelea kwenye ardhi yetu.” Amesema Judith Suminwa.
Wawakilishi hawa wamezungumza mbele ya Mkutano huo wa Umoja wa Mataifa huku kila upande ukitetea upande wake, wakati huu wakiendelea kulaumiana kuhusu ukosefu wa usalama mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.