Rais wa Iran awasili mjini New York, Marekani
Rais Masoud Pezeshkian wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amewasili mjini New York Marekani kwa ajili ya kuhudhuria mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.
Rais Pezeshkian aliondoka Tehran kuelekea New York asubuhi ya jana Jumanne na baada ya ndege yake kutua kwa muda mfupi nchini Algeria, aliendelea na safari yake na sasa amewasili New York.
Mheshimiwa Rais wa Iran anatarajiwa kuhutubia Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa leo Jumatano na vilevile atakuwa na mazungumzo ya ana kwa ana na viongozi wa nchi mbalimbali wanaohudhuria mkutano huo.
Kabla ya kuondoka hapa Tehran, Rais Pazeshkiani alisema kuwa, atatumia jukwaa la Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuzungumzia jinai kubwa zilizofanywa na Marekani nchini Iran ikiwa ni pamoja na kushambulia na kuua kwa umati watoto wadogo katika maeneo ya Minab na Lamerd nchini Iran.
Akijibu swali la mwandishi wa habari wakati akiwa ndani ya ndege, Rais Masoud Pezeshkian alisema kuhusu umuhimu wa kuhudhuria mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kwamba, anatumai kuwa kwa kuhudhuria kwake huko, walimwengu watapata kufahamu ukatili na jinai zinazoendelea kufanywa na madola ya kibeberu katika eneo la Asia Magharibi na kwa vile mkutano huo unafanyika kwa kaulimbiu ya 'imani' anatumai utaweza kurejeshe imani ya walimwengu kwa chombo hicho kikubwa zaidi duniani cha kimataifa na kutaongezeka jitihada za kukomesha vita na umwagaji damu duniani.
Alisema: "Tutaangazia hali ngumu ya watoto wetu huko Minab na Lamerd pamoja na ukatili wa wahusika wa jinai hiyo; binadamu hawafanyi vitendo kama hivyo, na tabia ya kikatili ya namna hiyo inasikitisha sana."