Sudan Kusini yabadilisha sheria kabla ya uchaguzi, wapinzani walalamika
Rais Salva Kiir wa Sudan Kusini ametia saini mabadiliko ya sheria yanayoondoa masharti ya kukamilisha katiba ya kudumu na sensa kabla ya uchaguzi wa Desemba, hatua ambayo imelalamikiwa vikali na muungano mkuu wa upinzani nchini humo.
Mabadiliko hayo yanalenga kufungua njia ya uchaguzi uliopangwa kufanyika Desemba 22 mwaka huu. Huo utakuwa uchaguzi wa kwanza nchini humo tangu Sudan Kusini ilipopata uhuru mwaka 2011 baada ya kujitenga na Sudan.
Muungano wa Upinzani wa Sudan Kusini, ambao ulitia saini makubaliano ya amani ya mwaka 2018, umeyakataa mabadiliko hayo. Umesema yamefanywa bila mashauriano ya kutosha baina ya pande zilizotia saini makubaliano hayo.
Mpinzani wa muda mrefu wa Kiir, Riek Machar, amekuwa katika kizuizi cha nyumbani tangu Machi 2025. Kiongozi huyo wa SPLM-IO anakabiliwa na mashtaka yakiwemo uhaini na mauaji, ambayo ameyakanusha. Wiki iliyopita, Kiir pia alimwondoa mkuu wa tume ya uchaguzi bila kueleza sababu.
Ofisi ya rais Kiir imesema marekebisho ya Sheria ya Uchaguzi ya mwaka 2012 ni hatua nyingine muhimu katika maandalizi ya uchaguzi. Waziri wa Masuala ya Rais, Africano Mande Gedima, amesema marekebisho hayo yanalenga kuifanya sheria hiyo iendane na katiba ya mpito.
Chini ya sheria mpya, viongozi waliopo madarakani wataendelea kutumia mamlaka yao kamili hadi rais mpya atakapoingia madarakani. Hata hivyo, makamu wa kwanza wa rais na makamu wengine wa rais wataondoka madarakani ndani ya miezi mitatu kabla ya siku ya uchaguzi.
Nchi hiyo changa zaidi barani Afrika ilitumbukia kwenye mapigano ya wenyewe kwa wenyewe mwezi Disemba 2013 baada ya Rais Salva Kiir wa nchi hiyo kumtuhumu makamu wake wakati huo, Machar kuwa alipanga njama ya kumpindua.