Mvua "za El Nino" zazua mafuriko, zaua watu 3 Libya
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i141698-mvua_za_el_nino_zazua_mafuriko_zaua_watu_3_libya
Watu watatu wa familia moja walifariki dunia jana baada ya gari lao kukombwa na mafuriko katika Wadi Zagar ya eneo la Milima Myeusi nchini Libya.
(last modified 2026-09-24T13:04:56+00:00 )
Sep 24, 2026 11:53 UTC
  • Mvua

Watu watatu wa familia moja walifariki dunia jana baada ya gari lao kukombwa na mafuriko katika Wadi Zagar ya eneo la Milima Myeusi nchini Libya.

Duru za ndani  za habari zimetangaza habari hiyo na kuongeza kuwa, gari hiyo ilikuwa na mwanamme mmoja, mkewe na binti yao na wote watatu wamefariki dunia baada ya gari yao kukumbwa na mafuriko hayo. Kituo cha Taifa cha Hali ya Hewa nchini Libya kilionya katika taarifa yake ya Jumatano kuhusu hali mbaya ya hewa itakayosababishwa na mvua kubwa na uwezekano wa kutokea mafuriko katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, dhoruba za radi na mvua kubwa zilitarajiwa kuyakumba maeneo ya kusini, katikati na magharibi mwa Libya na kusababisha mabonde kufurika na viwango vya maji kuongezeka katika maeneo ya nyanda za chini.

Siku chache zilizopita pia, shirika moja la kimataifa lilitahadharisha kuwa hali ya hewa ya El Niño inayozidi kuongezeka kwa kasi inatishia kuleta mafuriko makubwa, magonjwa na ukame katika maeneo la Afrika Mashariki na barani Asia.

Jumatatu wiki hiii, Kamati ya Kimataifa ya Uokoaji (IRC) iliarifu kuwa, Kenya, Uganda, Somalia, Bangladesh, Pakistan na Afghanistan ni miongoni mwa nchi zilizoko hatarini zaidi kukumbwa na mvua za El Nino.

Mwezi Julai mwaka huu pia Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO), lilitangaza kwamba hali ya El Niño tayari ilikuwa imeimarika na kwamba hali hiyo ilitabiriwa kuimarika kwa kasi kati ya Julai na Septemba.

El Niño ni mabadiliko ya asili ya halijoto katika Bahari ya Pasifiki ambayo hujirudia kila baada ya miaka miwili hadi saba, huku pepo zinazovuma kutoka mashariki kuelekea magharibii, kaskazini na kusini mwa Ikweta ambazo kwa kawaida husukuma maji ya uvuguvugu kuelekea magharibi, zikipungua na joto kuenea tena baharini.

Wiki iliyopita pia, Shirika la Kimataifa la Uhamiaji lilitangaza kwamba familia 168 zimelazimika kuhama makazi yao na nyumba 271 zimeharibiwa na mvua kubwa na mafuriko katika eneo la Abu Karshola la Jimbo la Kordofan Kusini, huko kusini mwa Sudan.