Iran yazindua teknolojia ya virusi vya kuangamiza saratani
-
Iran na teknolojia ya virusi ya kuangamiza saratani
Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imezindua teknolojia ya kiasili kwa ajili ya kubuni, uhandisi wa kijeni, uzalishaji wa virusi vya oncolytic vinavyoua seli za saratani.
Virusi hivi vina uwezo wa kuzaliana kwa kuchagua ndani ya seli za saratani, hatua inayofungua njia ya maendeleo ya tiba za kijeni na virusi kwa ajili ya saratani ambazo zimekuwa ngumu kutibiwa na njia za kawaida.
Teknolojia hiyo ilizinduliwa Jumapili katika hafla iliyoadhimisha kumbukumbu ya miaka 46 ya kuanzishwa kwa Akademia ya Elimu, Utamaduni, na Utafiti (ACECR), iliyofanyika katika Chuo cha Sayansi na Utamaduni cha ACECR mbele ya Rais Daktari Masoud Pezeshkian.
Mradi huu umendelezwa na Kikundi cha Utafiti cha Maendeleo ya Teknolojia ya Tiba ya Saratani katika Taasisi ya Kitaifa ya Saratani ya ACECR, chini ya uongozi mkuu wa taasisi hiyo, Daktari Ramin Saramifaroushani,
Mradi huu umeanzisha jukwaa la kwanza la kiteknolojia la ndani ya Iran kwa ajili ya kubuni, kufanya uhandisi wa kijeni, kuzalisha, na kusafisha virusi hivi. Katika hafla hiyo, Akademia ya Elimu, Utamaduni, na Utafiti ilitangaza pia kuanza kwa jaribio la kwanza la kimatibabu nchini Iran linalotumia teknolojia hiyo. Virusi vya oncolytic vimebuniwa kulenga seli za saratani pekee, kuzaliana ndani yake na kuziharibu huku vikipunguza athari kwa seli zenye afya, hivyo kutoa matumaini mapya kwa wagonjwa wanaosumbuliwa na saratani sugu.
Teknolojia hii inachukuliwa kuwa mbinu yenye matumaini makubwa kwa ajili ya kutibu saratani ambazo zimeshindikana kutibiwa. Mradi huu umekutanisha teknolojia za hali ya juu katika sayansi ya virusi (virology), uhandisi wa kijeni, bioteknolojia, na uzalishaji wa bidhaa za juu za kimatibabu (ATMPs).
Waziri wa Afya, Daktari Mohammad-Reza Zafarghandi, aliisifu kazi ya Akademia ya Elimu, Utamaduni, na Utafiti katika tiba na utafiti wa saratani, akielezea taasisi hiyo kama kiungo muhimu kati ya uwezo wa kisayansi na mahitaji ya kivitendo ya nchi.
Dkt. Zafarghandi pia amesisitiza nafasi ya akatemia hiyo katika kutoa fursa kwa watafiti na wataalamu vijana ambao uwezo wao unaweza kuzuiwa na vikwazo vya ukiritimba. Pia aligusia shughuli za Akademia ya Elimu, Utamaduni, na Utafiti katika maeneo mengine ikiwemo tiba ya utasa, seli shina (stem cells), na saratani kama mifano ya jitihada za wanasayansi Wairani ambazo zimechangia moja kwa moja katika kuboresha afya ya jamii na kuimarisha uhuru wa kisayansi wa taifa.