Alipoaga Dunia
-
Haram ya Mtume Muhammad (SAW) mjini Madina.
Tunafungua kipindi chetu kwa Hadithi maarufu ya Bwana Mtume (saw) ambayo madhumuni yake yamepokewa katika Hadithi nyingi zilizoandikwa na wanazuoni wa madhehebu mbalimbali za Kiislamu.
Imepokewa kwamba Mtume Muhammad (saw) amesema: "Nimekuachieni vizito viwili, hivyo tazameni jinsi mtakavyoamiliana navyo baada yangu, ambavyo ni Qur’ani na Ahlibaiti wangu. Mwenyezi Mungu Mjuzi ameniambia kwamba, havitatengana hadi vitakaponikuta mimi katika hodhi Siku ya Kiyama. Msiwatangulie Ahlulbaiti msije mkaangamia, wala msibaki nyuma msije mkahiliki. Msiwafunze lolote, kwani wao ni wajuzi kuliko ninyi." Hadithi hii imepokewa katika vitabu vingi marejeo kama Sahihi Muslim, Tirmidhi, Mustadraku al Sahihain, Khaswaisu Nasai na Tabaqati Ibn Saad.
Imepokewa pia kwamba, Mtume (saw) amesema: Enyi watu! Nimekubainishieni makimbilio yenu baada yangu, na imamu na kiongozi wenu ambaye ni Ali bin Abi Twalib. Yeye kwenu ni kama mimi baina yenu, mfuateni katika dini na mambo yenu yote. Hakika yeye ana elimu ya Kitabu cha Mwenyezi Mungu Mtukufu na hekima zake. Muulizeni na jifunzeni kutoka kwake na mawasii baada yake. Msiwatangulie wala kuachana nao, kwani wao wako pamoja na haki, na haki iko pamoja nao daima. XXXXX
Tunaendeleza simulizi zetu za leo kwa kisa kinachoonyesha tawaadhui na tabia ya kutopenda makuu ya Bwana wetu Muhammad (saw). Amesema: Alikuja kwangu Malaika ambaye hajawahi kuteremka kwa Nabii yeyote kabla yangu na wala hatateremkwa kwa mtu yeyote baada yangu; naye ni Malaika Israfil nikiwa pamoja na Malaika Jabrail na kusema: Assalamu alayka ya Muhammad. Kisha akasema: Mimi ni mjumbe wa Mola wako kwako wewe, ameniamuru nikupe khiari ya vitu viwili, ama uwe Mtume na mja wake, au uwe Mtume na mfalme. Mtume (saw) anasema nilichagua kuwa mtume na mja wa Mwenyezi Mungu (sw).
Mjukuu wa Mtume, Imam Ja'far Swadiq (as) pia anasema: Malaika Jabrail alimwendea Mtume mara tatu akiwa na funguo za hazina na utajiri wa ardhi na kumwambia kwamba, mali na utajiri huo wa dunia hautampunguzia lolote katika yale Mwenyezi Mungu aliyomtayarishia Siku ya Kiyama. Lakini Mtume alichagua kubakia mja na Mtumwa wa Mola wake Muumba. XXXCX
Imepokelewa kutoka kwa Imam Ja'far Swadiq, amani ya Mwenyezi Mungu iwe juu yake na babu zake kwamba amesema: “Watahinini Shia na wafuasi wetu kwa mambo matatu, nyakati za Swala jinsi wanavyozilinda na kuziheshimu, katika kulinda siri zao mbele ya maadui zetu, na katika mali zao, vipi wanawafariji ndugu zao kwa mali hizo.”
"إمْتَحِنوا شیعَتَنا عِنْدَ ثَلاثٍ؛ عِنْدَ مَواقیتِ الصّلاةِ کَیْفَ مُحافِظَتُهُمْ عَلَیْها وَعِنْدَ أسْرارِهِمْ کَیْفَ حِفْظُهُمْ لَها عَنْ عَدُوِّنا وَإلی أمْوالِهِمْ کَیْفَ مُواساتُهُم لاخْوانِهِمْ»؛ بحار الانوار، ج 83، ص22؛ جامع احادیث شیعه، ج4، ص58.
Amesema pia katika kutaja sifa za Shia na wafuasi wa Ahlul Bait (as) kwamba: “Shia na wafuasi wa kweli wa Ali (as) ni wale wanaolinda tumbo na tupu zao, wanaojipinda kwelikweli katika ibada na kumtumikia Mola wao, wakitarajia thawabu na malipo Yake, na kuogopa adhabu Yake. Ukiwaona hao basi ndio Shia na wafuasi wa Ja’far bin Muhammad.
«إنّما شیعَةُ عَلِیٍّ مَنْ عَفَّ بَطْنُهُ وَفَرْجُهُ واشْتَدَّ جِهادُهُ، وَعَمِلَ لِخالِقِه، وَرَجا ثَوابَهُ، وَخافَ عِقابَهُ، فإذا رَأیْتَ أولئکَ فَاُولئکَ شیعةُ جَعْفَرٍ" ؛ الکافی، ج2، ص233، ح9.
Tunaendelea na simulizi zetu za leo kwa Hadithi ya Imam Swadiq (as) akisimulia daraja za juu na Nabii na Bwana wetu Muhammad (saw). Anasema baadhi ya Makuraish walimuuliza Mtume, amani ya Mwenyezi Mungu iwe juu yake na Ali zake kwamba: Kwa kwa kitu gani umewatangulia mitume wote na kuwa bora mbele ya Mwenyezi Mungu kuliko wao, licha ya kwamba umetumwa ukiwa wa mwisho wao?
Mtume alisema: “Nilikuwa wa kwanza kukiri na kumkubali Mola Muumba aliyetukuka, na wa kwanza kumjibu wakati Mwenyezi Mungu alipochukua ahadi za Manabii wake wote na kuwauliza, Je si mimi Mola wenu? Wakasema ndiyo. Nilikuwa Nabii wa kwanza kusema ndio na kukubali, na hivyo nikawatangulia kukiri na kutamka kwamba, Yeye Mwenyezi Mungu, ndiye Mola wetu Mlezi.”
Anasema katika Hadithi nyingine kwamba: Malaika Jabrail aliteremka kwa Mtume Muhammad (saw) na kumwambia: Ewe Muhammad! Mola wako Mlezi anakusalimu na anasema: Hakika Mimi nimeharamisha Moto wa Jahannam kwa mgongo uliokuzaa, tumbo lililokubeba ukiwa mimba, na mwili uliokulea. Mgongo uliokuzaa ni wa baba yako yako, Abdullah bin Abdul Muttalib, na tumbo lililokubeba ni Amina bint Wahab, na mlezi wako ni Abu Twalib. XXXX
Imam Swadiq (sa) anaendelea kutusimulia Hadithi za babu yake na kutuelekeza kwa Mtume wa rehma na amani, Muhammad (saw) akitukataza kufanya jambo lolote linalomkera na kumuudhi Mtume wetu. Anasema kuwaambia masahaba zake kwamba: Kwa nini mnamkera na kumuudhi Mtume wa Mwenyezi Mungu?
Walimuuliza: Vipi tunamkera na kumuudhi? Imam Swadiq alisema: Hivi hamuelewi kwamba, matendo na amali zenu zinaonyeshwa kwake, na anapoona maasia katika amali hizo hukereka? Tazameni msije mkamkera Mtume wa Allah, na jitahidini kumfurahisha.” Vilevile imepokewa kwamba, Imam Swadiq (as) alikuwa akienda kwenye kaburi la babu yake, Mtume wa Mwenyezi Mungu Muhammad (saw), kisha anaweka mkono wake juu ya kaburi tukufu na kusema: “Ninamuomba Mwenyezi Mungu aliyekuteua, akakuongoza na kuwaongoza waja wake kupitia kwako wewe akuswalie.” Vilevile aliulizwa: Mwenyezi Mungu (sw) anawaamuru waja wake wamswalie Mtume na kujisalimisha kwake, vipi tutamswalia? Alisema: Semeni: Sala za Mwenyezi Mungu, Malaika, Manabii, Mitume na viumbe Wake wote zimshukie Muhammad na Aali zake, na amani ya Mwenyezi Mungu na rehma Zake zimwendee yeye na Aali zake. Maswahaba wake walimuuliza: Nini thawabu za kumswalia Mtume (saw)?
Alisema: Thawabu za mtu anayemswalia Mtume kama inavyotakikana ni kuondolewa katika dhambi na kuwa kama siku aliyozaliwa na mama yake.” XXXX
Siku Alipoaga Dunia
Wapenzi wasikilizaji, siku ambayo Mtume Muhammad (S.A.W.) alifariki dunia ilikuwa mojawapo ya siku zenye huzuni kubwa zaidi katika maisha ya Waislamu wote hususan Amirul Muminina, Ali (AS), Fatima Al Zahraa na watu wa familia ya Mtume. Mtume alipofariki dunia, kichwa chake kitakatifu kilikuwa mapajani mwa Ali bin Abi Twalib, huku nyumba ya Mtume ikiwa imejaa Muhajirina na Ansari.
Imamu Ali (a.s.) anasimulia katika Nahjul-Balagha kwamba alipofariki dunia Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) milango na kuta vilikua vikiomboleza na kulia kwa huzuni. Niliosha mwili wa Mtume nikisaidiwa na Malaika mbao walikuwa wakimswalia. Imam anaendelea kusimulia kwamba aliendelea kusikia sauti za Malaika wakimswalia Mtume bila kusita.
Ali (AS) aliosha na kuukafini mwili wa Mtume (S.A.W.); kwa sababu Mtume (S.A.W.) alikuwa ameagiza kwamba mtu wa karibu zaidi kwake ndiye atakayeosha mwili wake, na mtu huyo hakuwa mwingine ila Ali bin Abi Twalib. Kisha, Imam Ali (as) alifunua uso wa Mtume huku machozi yakimbubujika na kusema: "Baba na mama yangu watolewe kafara kwa ajili yako ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Kwa kifo chako, limekatika jambo ambalo halijawahi kukatika kwa sababu ya mauti ya mtu yeyote mwingine isipokuwa wewe; ambalo utume, wahyi na habari za mbinguni…. Lau kama usingeamuru uvumilivu na kukataza kukata tamaa, tungelia hadi machozi yetu yote yangekauka, maumivu yangeendelea na huzuni ingekuwa sahiba wetu wa kudumu, bali haya yote ni machache sana kwa ajili yako. Lakini kifo ni kitu ambacho hakuna mtu anayeweza kukizuia. Wazazi wangu wawe kafara yako. Tukumbuke mbele ya Mola wako na utuweke kwenye mazingatio yako.
Imam Ali (AS), akisaidiwa na watu wachache wa familia ya Mtume (S.A.W.), waliuzika mwili wake katika chumba alichofia, katika nyumba yake mwenyewe, kandokando ya msikiti aliouasisi yeye mwenyewe, ambao sasa unaitwa Msikiti wa Mtume mjini Madina.
Baada ya kuaga dunia Mtume, mitaa ya Madina ilinukia harufu ya upweke na uyatima. Vifua vilijaa huzuni kubwa na roho za watu zilikuwa zikiungua katika moto wa msiba. Fatima (SAW), binti kipenzi wa Mtume, alilia wakati wote na kumwita baba yake akisema: Waa abatah…. Waaaa Muhammadaah….. na tangu wakati huo hakuna mtu aliyemuona tena Mwanafatima akitabasamu hadi pale yeye mwenyewe alipoaga dunia na kumfuata baba yake katika Firausul Aalaaa. *********
Swala na salamu za Mwenyezi Mungu ziwe juu ya Mtume wetu Muhammad na Aali zake watoharifu, na tunamuomba Mwenyezi Mungu (sw) atujaalie miongoni mwa wanaomswalia Mtume Muhammad (SAW) na Aali zake na kutupa thawabu za wanaojua haki zao na kufuata mafundisho yao. Wassalamu alaykum warahmatullah wabarakatuh.