Mwezi 28 Safar, Siku aliyotawafu Bwana Mtume Muhammad SAW
https://parstoday.ir/sw/news/religion-i140624-mwezi_28_safar_siku_aliyotawafu_bwana_mtume_muhammad_saw
Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh wapenzi wasikilizaji. Mwezi 28 Safar, unasadifiana na kumbukumbu ya kut'awafu, yaani kuaga dunia Mtume wa Mwenyezi Mungu, Nabii Muhammad Al-Mustafa, rehma za Allah na amani Yake ziwe juu yake na Aali zake. Na kwa mujibu wa baadhi ya Hadithi, siku hiyo pia inasadifiana na kumbukumbu ya kufa shahidi mjukuu wake mpenzi, Imam Hassan al-Mujtaba AS.
(last modified 2026-08-12T13:45:36+00:00 )
Aug 12, 2026 13:24 UTC
  • Mwezi 28 Safar, Siku aliyotawafu Bwana Mtume Muhammad SAW

Assalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh wapenzi wasikilizaji. Mwezi 28 Safar, unasadifiana na kumbukumbu ya kut'awafu, yaani kuaga dunia Mtume wa Mwenyezi Mungu, Nabii Muhammad Al-Mustafa, rehma za Allah na amani Yake ziwe juu yake na Aali zake. Na kwa mujibu wa baadhi ya Hadithi, siku hiyo pia inasadifiana na kumbukumbu ya kufa shahidi mjukuu wake mpenzi, Imam Hassan al-Mujtaba AS.

Bwana Mtume Muhammad SAW, alikuwa mletaji ujumbe wa Mwenyezi Mungu kwa wanadamu, aliyeupamba ulimwengu kwa nuru ya imani, elimu na maadili.

Alizaliwa katika mji wa Makka, mwezi 17 Mfunguo Sita, Rabiul-Awwal katika Mwaka wa Tembo, sawa na mwaka 570 Miladia. Baba yake alikuwa Abdullah bin Abdul-Muttalib, na mama yake alikuwa Aaminah bint Wahab. Wote wawili walitokana na kabila kubwa la Quraysh.

Akiwa na umri wa miaka 40, Muhammad Al-Mustafa alibaathiwa na kupewa Utume. Na baada ya miaka 23 ya juhudi na Jihadi ya tablighi na ufikishaji ujumbe wa Mwenyezi Mungu, iliyoandamana na changamoto nyingi na misukosuko mikubwa, alifariki dunia katika mji wa Madina, akiwa na umri wa miaka 63.

Kaburi lake tukufu liko Madinatul-Munawwara, kando ya Msikiti wake, yaani Masjidu-Nnabiy, ambapo kila mwaka, umati usio na kifani wa maashiki, yaani watu wenye mapenzi naye makubwa mno kutoka kila pembe ya dunia, hususan katika masiku ya kabla na baada ya ibada ya Hija, huelekea huko Madina kwa ajili ya kumzuru mbora huyo wa viumbe.

Rehema na amani za Allah, ziishukie roho tukufu na takatifu ya mhitimishaji wa silisili ya Mitume, Nabii mteule Muhammad SAW.

Mahali lilipo kaburi tukufu la Bwana Mtume Muhammad SAW

 

Kwa muda wote wa karne nyingi zilizopita hadi sasa, ujumbe aliokuja nao mbora wa Mitume, Nabii Muhammad SAW, ambaye ndiye pia Mtume wa mwisho wa Mwenyezi Mungu umeziangazia kwa nuru ya Tawhidi, nyoyo za mamilioni kwa mamilioni ya watu wanaotafuta ukweli duniani kote na kuzitoa kwenye giza la ujinga na ujahilia na kuzipa uhai na utulivu wa kiroho na wa ulimwengu wa malakuti. Na hii ni pamoja na kwamba, akili za wanadamu bado hazijaweza kulidiriki ipasavyo, hata tone moja tu la chemchemi hiyo ya milele ya nuru ya uongofu.

Nabii Muhammad SAW, ni shakhsia ambaye neema ya uwepo wake na Utume wake vimewafungulia njia wanadamu ya kuifikia saada ya duniani na ukovu wa akhera; na ujumbe wake wa udugu, uadilifu, wa kulinda heshima ya mwanadamu, akhlaqi na maadili mema na kuwatetea wanyonge na waliodhulumiwa, ndivyo vinavyojenga misingi imara ya mafundisho na tunu aali na tukufu za Uislamu alizokuja nazo.

Yeye ni “Rahmatanun-Lil-aa'lamin” — yaani Rehema kwa walimwengu wote, na mletaji ujumbe wa upendo na urafiki kwa wanadamu wote, wa dini, matapo na makundi tofauti.

Kwa ushuhuda wa Historia, Mtume huyo wa Mwenyezi Mungu alikuwa na nafasi kubwa zaidi, muhimu zaidi na ya kipekee, katika kuleta mabadiliko kwenye maisha ya mwanadamu. Katika Aya ya 4 ya Suratul-Qalam, Mwenyezi Mungu Mtukufu anasema, Mtume aliyebaathiwa na kuchaguliwa kwa ajili ya jukumu hilo zito kabisa alikuwa amepambika kwa tabia na akhlaqi bora kabisa zilizomwezesha kuhimili na kuvumilia misukosuko mikubwa aliyokumbana nayo, na kusimama imara kuvishinda vizuizi na matatizo chungu nzima yaliyolenga kumkwamisha katika katika kazi ya kuwaelekeza watu kwenye uongofu.

Imam Khomeini, Mwenyezi Mungu amrehemu, ameandika yafuatayo katika kitabu chake kiitwacho Sharhe Hadise Jonude-Aql va-Jahl:

“Tabu kubwa zaidi na mateso mazito zaidi ambayo wamepata na wanayapata waongozaji wa njia ya haki ni kuamiliana na watu wajinga na kuwalingania watu wasio na ufahamu. Kwa hiyo, wao inapasa wapambike kwa tabia njema za kiwango cha juu kabisa, na inabidi nguvu ya kujenga urafiki, uhimilivu na mlahaka mwema, ya ndani ya nafsi zao, iwe ya namna itakayowawezesha kuhimili ujinga wa wajinga na wasio na busara.” Na hivyo, ndivyo alivyokuwa Mtume wetu mtukufu.

Moja ya vipengele muhimu vya shakhsia ya Bwana Mtume SAW, ni sira na mwenendo wake wa kukabiliana na maadui. Qur’ani Tukufu inasema katika Aya ya 29 ya Suratul-Fat’h: “Muhammad ni Mtume wa Mwenyezi Mungu; na wale walio pamoja naye, ni wakali kwa makafiri, na wanahurumiana wao kwa wao.”

Kwa mujibu wa Aya hii, inapasa Waislamu wawe wakali katika kukabiliana na adui na wala wasimruhusu kufanya vyovyote atakavyo dhidi yao.

Na kwa sababu hiyo, katika Aya ya 60 ya Suratul-Anfal, Mwenyezi Mungu Mtukufu anawaamrisha Waislamu wajizatiti na kujiweka tayari kwa hali zote ili kukabiliana na maadui; na kuandaa kila aina ya silaha, nyenzo, suhula na mbinu za tablighi na uenezi. Aya hiyo inasema: "Basi waandalieni nguvu kama muwezavyo, na kwa farasi walio fungwa tayari-tayari, ili kuwatishia maadui wa Mwenyezi Mungu na maadui zenu…”

Na ndio maana imepokewa katika historia, kwamba wakati Bwana Mtume SAW alipopata habari kuwa kuna silaha mpya imetengenezwa huko Yemen, alimtuma mtu akaifuatilie ili kuipata. Aidha imesimuliwa kwamba Mtukufu huyo amesema: (Kwa ajili ya kukabiliana na adui), watu watatu hupata thawabu za kuwapeleka Peponi kutokana na mshale mmoja: aliyeutengeneza, aliyeuandaa na aliyeufyatua.

Lakini pamoja na hayo, juhudi kubwa zaidi alizofanya Bwana Mtume SAW zilikuwa za kujenga umoja na udugu baina ya Waislamu. Kukabiliana na adui kunahitaji umoja. Kwa sababu hiyo, Bwana Mtume SAW alijitahidi kadiri ilivyowezekana kuzuia kuzuka vita na mapigano.

 

Lakini pale ilipotokezea upande wa pili kuvunja mikataba na kukhalifu ahadi na makubaliano, Mtukufu huyo alichukua hatua madhubuti kuzuia uchokozi na uvunjaji ahadi huo wa adui. Vita alivyopigana Bwana Mtume SAW na Mayahudi wa Madina vilitokana zaidi na sababu hiyo.

Baada ya kuhajiri Makka na kuhamia Madina, Mtukufu huyo aliongoza kwa mafanikio vita vingi vya Jihadi ambavyo Waislamu walilazimika kupigana na maadui wa Uislamu.

Alionesha kivitendo, kwamba kuilinda jamii ya Waislamu dhidi ya adui na kuongoza vita katika ngazi ya kamandi na ujemedari mkuu wa jeshi ni miongoni mwa majukumu ya mtawala wa Kiislamu.

Kuchunga haki za kiutu, kuwa na ushujaa na huruma, na kuwaenzi Mujahidina na familia za Mashahidi, ilikuwa ndio sira na mwenendo wa kimaadili wa Bwana Mtume SAW katika ukamanda na ujemedari wake wa vita.

Kuchukua maamuzi kwa uthabiti, kutotishika na silaha za adui na nyenzo zake za kidhahiri za vita, kushauriana na wapiganaji wake, kupanga na kuliandaa jeshi, pamoja na kutumia mbinu za kisaikolojia za vita, ilikuwa sehemu mojawapo ya sira za kijeshi za Bwana Mtume SAW katika vita kadhaa walivyopigana Waislamu na makafiri na maadui wa dini ya Mwenyezi Mungu.

Kwa mujibu wa Qur’ani Tukufu, Mtume wa Mwenyezi Mungu, rehema za Mola na amani yake ziwe juu yake na Aali zake, ni ruwaza na mfano mwema kwa wale wanaomwamini Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho, na kumdhukuru Yeye Mola kwa wingi.

Katika mafundisho aliyokuja nayo Nabii Muhammad SAW, watu wote wanastahiki heshima na haki, ambazo hazipaswi kuvunjwa, bila kujali rangi, kabila au hadhi zao katika jamii.

Bwana Mtume SAW alikuwa kila mara akiwalingania kwa msisitizo Waislamu kutekeleza uadilifu, kuwatetea waliodhulumiwa na kusimama imara dhidi ya dhulma. Akiwakumbusha kwamba, kunyamazia kimya uonevu na utovu wa haki na uadilifu si jambo linaloilaiki jamii ya watu wanaomwamini Mwenyezi Mungu.

Kwa maneno na matendo yake, alionesha kwamba, nguvu huwa na thamani, pale tu inapotumika kutetea haki, uadilifu na utu, na si kwa kufanyia uonevu na kwa ajili ya maslahi na manufaa ya binafsi.

Kwa hiyo, makamanda wa Kiislamu katika ngazi yoyote ile wanatakiwa pale wanapotumia mamlaka yao na kutekeleza majukumu yao, wamfanye Bwana Mtume SAW kuwa mfano na kigezo chao, hususan katika maadili ya ukamanda na uongozi.

 Na hasa hasa hii leo, -kutokana na tawala za kibeberu na kidhalimu kufanya kila aina ya jinai, unyama na ukatili ili kupora na kunyonya rasilimali za Waislamu-, Waislamu na watawala wa mataifa ya Kiislamu wanapaswa wawe macho na makini wasije wakahadaiwa na maadui; na wasimame imara kulinda maslahi na ardhi za Waislamu.

Hakuna shaka yoyote kuwa, hakuna jamii inayoweza kudumu kwa dhulma; na izza na heshima ya kweli inapatikana kwa kupigania uadilifu, kuheshimu utu wa mwanadamu na kuwatetea wanaodhulumiwa. Na huo ndio ujumbe wa Mtume wa Mwenyezi Mungu ambao leo hii pia unaweza kuwa mwenge wa kuongozea njia kwa wale wenye dhamira ya kujenga dunia ya haki na uadilifu zaidi, na ya utu na ubinadamu zaidi.

Katika siku za mwisho za uhai wake uliobarikiwa, Bwana Mtume Muhammad SAW alimtaka Bilal awaite watu wakusanyike msikitini. Akiwa katika hali ya ugonjwa, alitoa hotuba; kisha akawaambia watu, kama kuna mtu ana haki yoyote kwake yeye, ajitokeze kuidai. Hakukuwa na aliyejibu. Bwana Mtume akairudia kauli hiyo mara tatu; na ndipo sahaba mmoja aitwaye Ukkasha ibn Mihs'an akasimama na kusema, yeye anayo haki ya kudai. Ukkasha alimwambia Bwana Mtume: “Katika moja ya vita nilikuwa pamoja na wewe. Tulipokuwa tunarudi, ngamia wangu alimkaribia ngamia wako, na hapo fimbo yako ikanipiga kwenye tumbo.” Bwana Mtume akasema: “Ewe Bilal, ilete ile fimbo ili Ukkasha apate kulipiza kisasi cha haki yake.” Lakini wakati Ukkasha alipoonekana kuwa tayari kufanya hivyo, papo hapo alijitupa juu ya mwili wa Bwana Mtume, na kuanza kuubusu huku analia, na kumwambia amsamehe. Bwana Mtume, rehema za Allah na amani yake ziwe juu yake na Aali zake, akasema: “Ukkasha atakuwa sahibu yangu Peponi.”

Wapenzi wasikilizaji, siku aliyoaga dunia Bwana Mtume Muhammad SAW ilikuwa moja ya siku za majonzi na huzuni kubwa zaidi katika maisha ya Amirul-Mu’minin Ali, AS. Wakati Bwana Mtume anafumba jicho na kuiaga dunia, kichwa chake kitukufu kilikuwa mapajani mwa Ali AS, huku nyumba yake ikiwa imejaa masahaba zake wa Muhajirina na Ansar. Katika Nahjul-Balagha, Imam Ali AS anasema: "Alipotawafu Mtume wa Allah, kila kitu kililia na kuomboleza. Mimi ndiye niliyeushughulikia kuuosha mwili wa Mtume, huku Malaika wakinisaidia na pia wakamsalia. Masikio yangu hayakuacha kusikia sauti zao za chini wakati walipokuwa wanamsalia".

Msikiti Mtukufu wa Bwana Mtume Muhammad SAW 

 

Imam Ali AS aliuosha na kuuvisha sanda mwili mtukufu na mtoharifu wa Bwana Mtume Muhammad SAW. Na sababu ni kuwa, yeye Mtume alikuwa ameshausia, aoshwe na mtu wake wa karibu zaidi; na bila shaka mtu huyo asingekuwa mwingine ghairi ya Ali. Baada ya kukamilisha yote hayo, Imam Ali aliufunua uso wa Bwana Mtume, na huku machozi yanambubujika akasema: “Baba na mama yangu wawe mhanga kwa ajili yako! Kwa kifo chako, limekatika jambo ambalo halijakatika kwa kifo cha mtu mwingine yeyote: ni kumalizika wito wa Mitume na kukatika habari za mbinguni. Kifo chako kimewafanya waliopatwa na msiba walazimike kuwa na uvumilivu na kimewaunganisha wote katika maombolezo haya… Lau isingekuwa umetuamrisha kuwa na subira na uvumilivu, ningelia mpaka chemchemi ya machozi ikauke. Majonzi haya na kilio chetu kwa msiba wa kuondoka kwako ni madogo, lakini mauti hayawezi kurudishwa nyuma, wala mtu hawezi kuepukana nayo. Baba na mama yangu wawe mhanga kwa ajili yako; utukumbuke mbele ya Mola wako na utuhifadhi kwenye kumbukumbu yako.”

Ali AS alimzika Bwana Mtume Muhammad SAW, -jua hilo la uongofu ling'aralo-, kwenye chumba kilekile alichofia, ndani ya nyumba yake iliyokuwa jirani na msikiti aliouasisi yeye mwenyewe, ambao leo hii unajulikana kama Masjidun-Nabiy.

Baada ya kuaga dunia Bwana Mtume, mitaa na vichochoro vya mji wa Madina viligubikwa na wingu zito la ukiwa na uyatima. Nyoyo zilijaa majonzi makubwa, na roho za watu zilikuwa zikiungulika na kuteketea kwa maumivu ya msiba huo mkubwa. Bibi Fatimatu-Zahra SA, binti kipenzi cha Mtume, aliendelea kumiminikwa na machozi na kumuita baba yake. Baada ya msiba huo, tabasamu halikuonekana tena kwenye uso wa bibi huyo mtukufu.

Wapenzi wasikilizaji, nachukua fursa hii kukupeni mkono wa pole Waislamu nyote na kila anayempenda Bwana Mtume Muhammad SAW kwa mnasaba huu, wa kukumbuka siku mbora huyo wa viumbe alipotawafu na kurejea kwa Mola wake. Wassalamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh…/