Aug 12, 2026 03:44 UTC
  • Jumatano, Agosti 12, 2026

Leo ni Jumatano tarehe 28 Mfunguo Tano Safar 1448 Hijria inayosadifiana na tarehe 12 Agosti 2026.

Siku kama ya leo miaka 1437 iliyopita inayosadifiana na tarehe 28 Safar mwaka 11 Hijria, alifariki dunia Mtume Muhammad (saw) akiwa na umri wa miaka 63.

Kutokana na kuwa na tabia ya ukweli na uaminifu tangu alipokuwa na umri mdogo, Mtume Mtukufu (saw) alipata umashuhuri kwa jina la "Muhammad Mwaminifu". Akiwa na umri wa miaka 40 Mwenyezi Mungu SW alimteua kuwa Mtume Wake ili aweze kuwalingania watu ibada ya Mungu Mmoja na kuondoa ukabila, dhulma na ujinga.

Watu wa dini, madhehebu na mirengo tofauti na hata wale wasiokuwa na dini kabisa wamesema mengi kuhusu shakhsia adhimu ya Nabii Muhammad (saw). Mwandishi wa Ulaya, Stanley Lane Poole ameandika kwamba, Mtume Muhammad alipendwa na watu wote na kila aliyemuona, na kwamba hajawahi kuona wala hatamuona tena mtu mithili yake.    ****

Siku kama ya leo miaka 1398 iliyopita, yaani sawa na tarehe 28 Safar mwaka 50 Hijiria, aliuawa shahidi Imam Hassan bin Ali bin Abi Twalib al Mujtaba (as), mjukuu wa Mtume Mtukufu (saw).

Imam Hassan (as) ni mtoto wa Bibi Fatima al Zahra na Imam Ali bin Abi Talib (as), na alizaliwa mwaka wa 3 baada ya Mtume (saw) kuhamia mjini Madina. Mtukufu huyo aliishi miaka saba ya mwanzo ya umri wake pamoja na babu yake Mtume Muhammad (saw) ambapo alinufaika na mafunzo na maarifa ya dini Tukufu ya Kiislamu.

Imam Hassan alichukua jukumu zito la kuongoza Umma wa Kiislamu akiwa na umri wa miaka 37 baada ya kuuawa shahidi baba yake, Imam Ali (as). Baada ya kuuawa shahidi Imam Ali (as) Waislamu walimpa baia Imam Hassan kwa ajili ya kuwaongoza, ambapo hata hivyo baada tu ya kuteuliwa kwenye nafasi hiyo alikabiliwa na njama pamoja na ukwamishaji mambo wa Muawiyah bin Abi Sufiyan.

Hatimaye Imam Hassan aliandaa jeshi aliloachiwa na baba yake kwa ajili ya kumkabili Muawiya, ingawa muovu huyo (Muawiya) alitumia hila za kila namna kuwanunua wafuasi wa Imam Hassan ambao hatimaye walimkimbia na kumwacha peke yake mjukuu huyo wa Mtume wa Allah. Imam Hassan aliuawa shahidi siku kama ya leo kwa kupewa sumu katika njama iliyopangwa na Muawiya bin Abi Sufyan.  ***

Tarehe 12 Agosti mwaka 1949 hati ya makubaliano ya kimataifa ya kuwalinda majeruhi na mateka wa kivita ilipasishwa kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa huko Geneva, Uswisi.

Hati hiyo ilibuniwa kufuatia miamala isiyo ya kibinadamu na jinai zilizokuwa zikifanywa dhidi ya majeruhi na mateka wa kivita wakati wa Vita vya Pili vya Dunia.    *****

Siku kama hii ya leo miaka 49 iliyopita sawa na tarehe 12 Agosti 1976, kambi ya wakimbizi wa Palestina ya Tel al Zaatar iliyoko karibu na Beirut mji mkuu wa Lebanon, ilitekwa baada ya kuzingirwa kwa muda mrefu na wanamgambo wa Kimaroni wa nchi hiyo na wakazi wake wakauawa kwa umati.

Kambi hiyo ilikuwa ikiwahifadhi maelfu ya wakimbizi wa Palestina na ilianza kuzingirwa mwanzoni mwa mwaka 1976 kwa uungaji mkono na uingiliaji wa utawala wa Kizayuni wa Israel. Utawala wa Kizayuni ulifanya hivyo kwa lengo la kushadidisha vita vya ndani huko Lebanon.  ****

Na miaka 27 iliyopita, Umoja wa Mataifa uliitangaza Agosti 12 kila mwaka, kuwa ‘Siku ya Vijana Duniani’ ili kueleza umuhimu wa vijana katika dunia ya sasa.

Tabaka hili lenye utanashati la jamii ndiyo sababu ya maendeleo ya kila nchi kwa msingi huo vijana katika kila nchi wanapaswa kupewa umuhimu mkubwa. Kutokana na umuhimu wao vijana wanapaswa kulindwa na kusaidiwa na serikali hususan katika masuala ya ajira, makazi na kujenga familia.

Katika upande mwingine kizazi cha leo cha vijana kinakabiliwa na changamoto nyingi za kimwili na kiroho ikiwa ni pamoja na ongezeko la matumizi ya dawa za kulevya, magonjwa ya kuambukiza kama Ukimwi na virusi vya HIV, intaneti na michezo ya computa ambayo inawatumbukiza vijana wengi katika ufuska na utovu wa maadili.

Kutangazwa Siku ya Vijana Duniani kunaweza kusaidia juhudi za kuwakumbusha vijana umuhimu wao na kuzuia changamoto mbalimbalizinazolikabili tabaka hilo muhimu.