Jumamosi, Septemba 19, 2026
Leo ni Jumamosi 7 Mfunguo Saba Rabiuthani 1448 Hijria mwafaka na 19 Septemba 2026 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 216 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria Abul-Feidh Hamdun Ibn Abdul-Rahman mashuhuri kwa jina la Ibn Haj, mfasiri, mwanafasihi na fakihi wa Kiislamu aliaga dunia. Alizaliwa mwaka 1174 Hijria katika moja ya miji ya leo ya Morocco na kukulia huko. Ibn Abdul-Rahman alisoma elimu za fasihi na dini kwa walimu na maustadhi mashuhuri wa zama hizo. Alimu na mwanazuoni huyu alikuwa mahiri pia katika uandishi wa vitabu ambapo ana vitabu mbalimbali katika elimu za fikihi, teolojia, tafsiri, mantiki na elimu nyigine.
***
Miaka 119 iliyopita, katika siku kama ya leo, tarehe 19 Septemba 1907: Kwa mara ya kwanza katika historia ya juhudi za mwanadamu za kupata nishati na malighafi zinazozalisha joto, mafuta ya sanisi yaliyotengenezwa kutokana na makaa ya mawe. (synthetic oil) yalizalishwa. Nyenzo hiyo mpya ya kuzalisha joto iligunduliwa na James Young, mwanakemia kutoka Scotland. Young alikuwa mmiliki wa mgodi mkubwa wa makaa ya mawe pamoja na maabara yenye vifaa vya kutosha. Kupitia mchakato wa uyeyushaji na utenganishaji wa makaa ya mawe kwa njia ya kunereka (distillation), alifanikiwa kuzalisha mafuta ya sanisi yaani ya kutengenezwa kiwandani.
***
Katika siku kama ya leo miaka 68 iliyopita, serikali ya kwanza huru iliundwa na viongozi wa mapinduzi nchini Algeria. Harakati za wananchi wa Algeria dhidi ya mkoloni Mfaransa zilianza mwanzoni wa Novemba 1954 sambamba na kushika kasi harakati za kupigani uhuru za wananchi hao. Nalo Jeshi la Ukombozi wa Algeria likaundwa kwa shabaha ya kuratibu mapambano. Tarehe 19 Septemba mwaka 1958 serikali ya muda ya Algeria ikatangaza uwepo wake. Hatimaye kushindwa jeshi la Ufaransa kusambaratisha harakati ya wananchi wa Algeria, kulipelekea Algeria ijitangazie uhuru mwaka 1962.
***
Siku kama ya leo miaka 35 iliyopita, Kuwait na Marekani zilisaini makubaliano ya kijeshi. Makubaliano hayo yalisainiwa karibu miezi sita baada ya Iraq kuhitimisha kuikalia kwa mabavu Kuwait. Viongozi wa Kuwait walidai kwamba, lengo la makubaliano hayo, ni kuzuia kutokea tena uvamizi mwingine wa Iraq dhidi ya nchi hiyo. Kwa mujibu wa makubaliano hayo ya kijeshi, Marekani iliruhusiwa kutumia bandari za Kuwait na kutuma wanajeshi na zana zake za kijeshi katika ardhi ya nchi hiyo na nchi mbili hizo kufanya mazoezi ya pamoja ya kijeshi. Mwaka 1991, Kuwait ikatiliana saini makubaliano kama hayo na Uingereza na Ufaransa. Miaka iliyofuatia, Bahrain, Qatar, Oman na Umoja wa Falme za Kiarabu zilisaini makubaliano ya kijeshi na Marekani, Uingereza na Ufaransa. Hata hivyo kinyume na matarajio ya viongozi wa nchi hizo za Ghuba ya Uajemi, makubaliano hayo badala ya kuwaletea amani, yalipelekea kutokea ushindani wa kumiliki silaha na kushadidi ukosefu wa amani katika Mashariki ya Kati.
***
Na miaka 32 iliyopita katika siku kama ya leo, wanajeshi elfu 20 wa Marekani walifanya mashambulizi ya anga na baharini na kuikalia kwa mabavu nchi ndogo ya Haiti inayopatikana katika bahari ya Caribean huko kusini mwa Marekani. Washington ilidai kuwa imeishambulia Haiti ili imrejeshe madarakani Rais Jean Bertrand Aristide wa nchi hiyo. Mwezi Septemba mwaka 1991 Jenerali Raoul Cedras alimpindua Aristide ambaye ndio kwanza alikuwa uongozini kwa muda wa miezi minane. Baada ya mapinduzi hayo Rais Jean Bertrand Aristide alikimbilia Marekani.
***