Jumamosi, 10 Oktoba, 2026
-
Leo Katika Historia
Leo ni Jumamosi 28 Mfunguo Saba Rabiuthani 1448 Hijria ambayo inasadifiana na 10 Oktoba 2026 Miladia.
Miaka 810 iliyopita katika siku sawa na ya leo Abubakar Muhyiddin Muhammad mashuhuri kwa jina la Ibnul Arabi, arifu na msomi mkubwa wa Kiislamu aliaga dunia huko Damascus. Alizaliwa mwaka 560 Hijria huko Andalusia, Uhispania ya leo. Ibn Arabi alifanya safari nyingi katika baadhi ya nchi na miji ikiwemo Tunisia, Makka, Halab (Aleppo) na Baghdad, na kila alipofika aliheshimiwa na kukirimiwa. Ibn Arabi alikuwa msomi hodari na baadhi ya duru zinasema kuwa ameandika vitabu na risala zaidi ya 500. Miongoni mwa kazi zake kubwa ni vitabu vya "Tafsir Kabir", "al-Futuhatul Makkiyyah" na "Fususul Hikam".
***
Miaka 295 iliyopita katika siku kama ya leo, alizaliwa huko katika mji wa Nice Ufaransa, Henry Cavendish mwanafalsafa na tabibu wa Kiingereza. Cavendish alikuwa mwalimu wa masomo ya fikizikia na kemia. Henry Cavendish alikuwa mtu wa kwanza aliyethibitisha kuwa gesi ya hyadrogen ni nyepesi zaidi kuliko hewa ya kawaida. Cavendish aliaga dunia mwaka 1810.
***
Tarehe 10 Oktoba miaka 146 iliyopita, kuliundwa muungano wa nchi tatu za Austria, Ujerumani na Italia. Kabla ya Italia kujiunga na muungano huo, awali kulikuwa na muungano wa mihimili miwili kati ya Austria na Ujerumani. Moja ya vipengee vya muungano huo kilikuwa na kusaidiana nchi wanachama pindi mmoja wao atakaposhambuliwa. Muungano huo ulikuwa ukiongezewa muda kila baada ya miaka mitano.
***
Katika siku kama ya leo miaka 114 iliyopita, mfumo wa Jamhuri nchini China ulichukua hatamu baada ya kuangushwa mfumo wa Kifalme. Katika kipindi cha kati ya mwaka 1907 na 1911 kulitokea uasi mara tano nchini China dhidi ya familia ya Kifalme ya Manchu. Uasi wote huo chimbuko lake kwa namna moja au nyingine lilikuwa ni fikra za kimapinduzi za Sun Yat-Sen mwanamapambano mashuhuri wa China. Hata hivyo uasi wa tano ambao ulianza tarehe 9 Oktoba mwaka 1911 ulipelekea kutokea ukandamizaji mkubwa, kutiwa mbaroni watu na mamia ya wengine kunyongwa hali ambayo ililipua ghadhabu na hasira za watu.
***
Siku kama ya leo miaka 56 iliyopita, nchi ya Fiji ilipata uhuru kutoka kwa Uingereza na siku kama hii husherehekewa nchini humo ikijulikana kama siku ya taifa. Fiji ilikuwa koloni rasmi la Uingereza tangu mwaka 1874 na Uingereza iliendelea kuukoloni muungano wa visiwa vya Fiji na ukoloni huo uliendelea kwa zaidi ya miaka 90. Mwaka 1965 katiba mpya ilianza kutekelezwa huko Fiji ambapo sheria zilibuniwa kwa ajili ya kupigania mamlaka ya kujitawala nchi hiyo.
***