Jumatano, 7 Oktoba, 2026
-
Leo Katika Historia
Leo ni Jumatano mwezi 25 Mfunguo Saba, Rabiuthani 1448 Hijria, sawa na tarehe 7 Oktoba, 2026 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 77 iliyopita, Ujerumani ya Mashariki iliasisiwa na kuwa na mfumo wa Jamhuri ya Kidemokrasia. Katika miezi ya mwishoni mwa Vita vya Pili vya Dunia, Shirikisho la Umoja wa Sovieti liliivamia na kuikalia kwa mabavu ardhi ya Ujerumani ya Mashariki, na madola ya Magharibi yakadhibiti sehemu ya magharibi mwa nchi hiyo. Hata hivyo baadaye Umoja wa Sovieti ulijitoa katika Baraza la Makamanda Waitifaki baada ya kutofautiana na madola ya Magharibi juu ya namna ya kuiendesha nchi hiyo.
&&&
Miaka mitatu iliyopita katika siku kama ya leo, Harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina HAMAS ilitekeleza operesheni ya kushtukiza kwa kupenya ndani ya ardhi ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu (Israel). Operesheni hiyo iliyojulikana kwa jina la Kimbunga cha al-Aqsa ilipelekea kuchukuliwa mateka makumi ya Wazayuni. Operesheni ya Kimbunga cha al-Aqsa ilitekelezwa wakati ambapo Israel ilikuwa katika harakati za kuanzisha uhusiano wa kawaida na baadhi ya mataifa ya Kiarabu. Israel ikiwa na lengo la kujibu operesheni ya Hamas ilianzisha hujuma kubwa ya kijeshi ya anga na baharini dhidi ya Ukanda wa Ghaza. Katika kipindi hiki cha miaka mitatu, Waziri Mkuu wa utawala wa kizayuni wa Israel Benjamin Netanyahuu na serikali yake wamefanya mauaji makubwa ya kimbari katika Ukanda wa Ghaza. Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC imetoa waranti wa kutiwa mbaroni Netanyahu kwa kutenda jinai za kivita.
&&&
Siku kama ya leo miaka 205 iliyopita mji wa Yerevan uliangukia mikononi mwa vikosi vya Urusi wakati wa kujiri vita vya pili kati ya dola hilo na Iran. Mji huo ulitekwa katika zama za utawala wa Fat'h Ali Shah Qajar na ukakabidhiwa kwa Warusi. Matokeo ya kushindwa huko kukawa ni kusainiwa mkataba wa Turkmenchay (Treaty of Turkmenchay). Kwa mujibu wa mkataba huo na kutokana na udhaifu wa Shah Qajar, sehemu kubwa ya ardhi ya kaskazini mwa Azerbaijan na Caucasia ilitengwa na ardhi ya Iran na kuunganishwa na Urusi.
&&&
Siku kama ya leo miaka 25 iliyopita yaani tarehe 7 Oktoba 2001, Marekani iliivamia Afghanistan. Uvamizi huo ulifanyika kwa kisingizio cha kuliangamiza kundi la wanamgambo wa Al-Qaida ambao kwa mujibu wa Washington lilihusika na tukio la Septemba 11 mwaka 2001 nchini Marekani. Katika kipindi cha wiki kadhaa, ndege za kivita za Marekani, zilifanya mashambulizi dhidi ya ngome za kundi la Taliban ambalo katika kipindi hicho lilikuwa likidhibiti eneo kubwa la ardhi ya Afghanistan sambamba na kuliunga mkono kundi la Al-Qaida lililokuwa likiongozwa na Osama bin Laden. Mashambulizi hayo makali ya Marekani yaliua na kujeruhi maelfu ya raia wasio na hatia wa Afghanistan huku wengine wakilazimika kuwa wakimbizi.
&&&
Na siku kama ya leo miaka 98 iliyopita, yaani tarehe 7 Oktoba 1928, Sohrab Sepehri malenga na mchoraji wa Kiirani alizaliwa katika mji wa Kashan moja ya miji ya katikati mwa Iran. Mwaka 1951 Sepehri alitoa majimui ya kwanza ya tungo zake za mashairi zilizoitwa "Marge Rang" na akatoa tena majimui nyingine ya vitabu vinane. Aidha mbali na Sohrab Sepehri kuwa malenga mkubwa, alipendelea sana taaluma ya uchoraji. Miongoni mwa athari za Sepehri ni pamoja na majimui za vitabu vya mashairi vinavyoitwa "Zendegi Khob'ha", "Musafir" na "Aavaz Oftaab." Sohrab Sepehri alifariki dunia mwaka 1980 na kuzikwa mahali alipozaliwa yaani mjini Kashan…/