Oct 05, 2026 02:45 UTC
  • Leo Katika Historia
    Leo Katika Historia

Leo ni Jumatatu 23 Mfunguo Saba Rabiuthani 1448 Hijria mwafaka na 5 Oktoba 2026 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 849 iliyopita yaani tarehe 23 Rabiuthani mwaka 599 Hijria alizaliwa huko Damascus Shihabuddin Abdulrahman Dimashqi al-Maḳdisī maarufu kwa lakabu ya Abu Shama. Alikuwa mwanashistoria wa Kiarabu na alikuwa miongoni mwa walimu walioheshimika wa skuli za Damascus. Abdulrahman Dimashqi alielekea Alexandria nchini Misri baada ya masomo yake ya awali; na akiwa katika mji huo alijifunza hadithi, fiqhi na maarifa mengine ya zama hizo. Aidha kwa muda fulani alikuwa mkuu wa Darul Hadith Ashrafiyya.Vitabu kwa majina ya "Utangulizi wa Sarufi" na "Muhtasari mfupi wa Historia ya Damascus" ni miongoni mwa kazi za msomi huyo mkubwa. 

***

Miaka 203 iliyopita katika siku kama ya leo, Allamah Ahmad Naraqi, faqihi, mwanahadithi na mshairi mashuhuri wa Iran, alifariki dunia. Allamah Ahmad Naraqi alizaliwa mwaka 1185 Hijria. Katika kipindi cha ujana wake, alisoma elimu mbalimbali za Kiislamu katika mji wa Kashan, ulioko katikati mwa Iran, chini ya uangalizi wa baba yake aliyekuwa mwanazuoni mashuhuri na mwenye heshima, Mulla Mahdi Naraqi. Kutokana na juhudi zake katika kutafuta elimu, alifikia daraja ya juu ya Ijtihadi. Baadaye, Allamah Naraqi alikwenda katika mji wa Najaf nchini Iraq, ambako alikaa kwa miaka kadhaa akisoma na kujifunza kwa wanazuoni mashuhuri wa wakati huo. Baada ya kifo cha baba yake, Allamah Naraqi alirejea Kashan na kuchukua nafasi ya baba yake katika uongozi wa Hawza ya Kiislamu ya mji huo, pamoja na kushika jukumu la uongozi wa kidini wa Waislamu katika maeneo mbalimbali ya Iran. Mwanazuoni huyo aliyesifika kwa uchamungu na elimu, ameacha vitabu na maandiko mbalimbali. Miongoni mwa kazi zake mashuhuri ni “Miraj al-Sa'adah”, “Asrar al-Hajj”, pamoja na “Mathnawi Taqdis”, kitabu kinachojumuisha mashairi yenye maudhui ya kiroho na kiirfani.

***

Katika siku kama ya leo miaka 162 iliyopita, alizaliwa Louis Jean Lumiere, mwanakemia mashuhuri wa Kifaransa. Mwaka 1895 akiwa pamoja na ndugu yake aliyejulikana kwa jina la Auguste Lumiere, walifanikiwa kutengeneza kifaa ambacho kiliwasaidia kuchukua picha mbalimbali na kusajili harakati. Mwaka huo huo Lumiere alifanikiwa kuonyesha filamu yake ya kwanza au Motion Picture katika majumba ya sinema. 

***

Miaka 48 iliyopita katika siku kama ya leo Imam Khomeini (MA) mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aliondoka Iraq na kuhamia Paris, Ufaransa. Imam Khomeini aliamua kufanya hijra hiyo ya kihistoria wakati utawala wa zamani wa Iraq ulipoanza kumzuia kufanya harakati za mapambano dhidi ya utawala wa Shah. Serikali ya wakati huo ya Iraq ambayo ilikuwa ikilinda uhusiano wake na utawala wa Shah nchini Iran, ilimtaka Imam Khomeini ajiepushe na harakati zozote za kisiasa na za kimapinduzi dhidi ya utawala huo wa Shah. Hata hivyo Imam aliiambia serikali hiyo kuwa hilo lilikuwa jukumu lake la kisheria ambalo aliwajibika kulitekeleza na kusisitiza juu ya kuendelezwa mapambano kwa kutoa hotuba na kutuma kanda za kimapinduzi nchini Iran. 

***

Siku kama ya leo miaka 25 iliyopita, Slobodan Milosevic dikteta wa zamani wa Yugoslavia na mhusika mkuu wa vita vya umwagaji damu huko Balkan, alijiuzulu baada ya miezi kadhaa ya malalamiko ya ndani na vikwazo vya kimataifa. Milosevic alikuwa rais wa Serbia tangu mwaka 1990 hadi 1997 na baadaye akawa Rais wa Jamhuri ya Yugoslavia. Katika vita vya Bosnia, na kwa uungaji mkono wa kila upande wa Waserbia, Slobodan Milosevic alishiriki pakubwa katika kutekeleza mauaji ya kizazi dhidi ya Waislamu wa Bosnia Herzegovina. Milosevic alikuwa kiongozi wa kwanza mtenda jinai za kivita kufikishwa katika Mahakama ya Kimataifa kwa ajili ya kuhukumiwa. Hata hivyo mhalifu huyo katili alifariki dunia akiwa katika korokoro za mahakama hiyo huko The Hague nchini Uholanzi kutokana na mwendo wa kinyonga wa kushughulikia kesi yake. 

***

Tarehe 5 Oktoba ni Siku ya Kimataifa ya Mwalimu. Siku hii ilitangazwa kuwa ni Siku ya Kimataifa ya Mwalimu katika kikao cha Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kilichofanyika tarehe 3 hadi 8 mwezi Septemba mwaka 1994. Lengo la kutangazwa siku hii ni kwa ajili ya kuenzi mchango wa walimu na nafasi yao kubwa katika jamii ya mwanaadamu. 

***