Jumamosi, 03 Oktoba 2026
Leo ni Jumamosi 21 Mfunguo Saba Rabiuthani 1448 Hijria mwafaka na 03 Oktoba 2026 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 76 iliyopita (21 Rabiu-Thani, 1371 Hijria Qamaria), aliaga dunia mwanachuoni mkubwa wa zama hizo, Ayatullah Muhammad Nahavandi. Ayatullah Muhammad Nahavandi, mwana wa mwanazuoni mchamungu Ayatullah Mirza Abdul Rahim Nahavandi, alizaliwa Najaful-Ashraf nchini Iraq. Kama alivyokuwa baba yake, Ayatullah Nahavandi anatambuliwa kuwa mmoja wa wasomi na wanazuoni wakubwa wa karne ya 14 kwa ubobezi wake katika elimu, matendo, na maadili. Miongoni mwa athari zilizoachwa na alimu huyo ni tafsir ya al-Mabsut ya Kiarabu na Kifarsi na mkusanyiko wa vitabu viwili katika juzuu 4, viitwavyo Nafahaatu-Rahman.
***
Katika siku kama ya leo miaka 159 iliyopita, wawakilishi wa Italia na utawala wa kifalme wa Austria walisaini Mkataba wa Vienna katika mji unaojulikana kwa jina hilo. Kwa mujibu wa mkataba huo, Austria iliikabidhi Italia jimbo la Venice. Moja kati ya vipengee muhimu vya mkataba wa Vienna kilikuwa ni hiki kwamba, utawala wa kifalme wa Austria upigwe marufuku kuingilia masuala ya ndani ya Italia. Mkataba wa Vienna ulifungua njia ya kuungana Italia mwaka 1870.
***
Miaka 94 iliyopita katika siku kama ya leo Iraq ilipata uhuru kutoka kwa mkoloni Muingereza. Iran iliiweka Iraq chini ya mamlaka yake mwaka 539 kabla ya kuzaliwa Nabii Issa (A.S). Iraq ilikuwa sehemu ya utawala wa kifalme wa Iran hadi ardhi hiyo ilipokombolewa na Waislamu mwaka 642 Miladia. Iraq iliendelea kudhibitiwa na utawala huo wa kifalme hadi mwishoni mwa utawala wa Bani Ummayya na mji wa Baghdad ulichaguliwa kuwa makao makuu sambamba na kuingia madarakani utawala wa Bani Abbas.
***
Tarehe 3 Oktoba miaka 84 iliyopita kombora la kwanza lililotengenezwa na mwanadamu lilirushwa angani. Wernher von Braun alikuwa miongoni mwa wataalamu wa makombora wa Ujerumani ambao baada ya kuanza Vita vya Pili vya Dunia jeshi la nchi hiyo lilimpa jukumu la kutengeneza kombora la kwanza. Tarehe 3 Oktoba mwaka 1942 kundi la wataalamu wa Ujerumani lilifanikiwa kurusha angani kombora hilo lililokuwa na urefu wa mita 14 na uzito wa karibu tani 13. Kombora hilo lilirushwa angani katika Bahari ya Baltic.
***
Siku kama ya leo miaka 36 iliyopita, ilitangazwa rasmi habari ya kuungana tena Ujerumani ya Mashariki na Ujerumani ya Magharibi na nchi mbili hizo kwa mara nyingine tena zikaunda Ujerumani moja baada ya miaka 45 ya kutengana. Baada ya kushindwa Ujerumani katika Vita vya Pili vya Dunia, eneo la mashariki mwa Ujerumani lilikaliwa kwa mabavu na Urusi ya zamani na lile la magharibi likadhibiwa na nchi za Magharibi. Nchi mbili za Ujerumani ya Magharibi na ya Mashariki zilitangazwa kuasisiwa mwaka 1949 kwa kuwa na mifumo miwili tafauti ya kisiasa na kiuchumi.