Oct 02, 2026 02:43 UTC
  • Ijumaa, Oktoba 2, 2026

Leo ni Ijumaa, mezi 20 Mfunguo Saba Rabiuth Thani 1448 Hijria sawa na tarehe Pili Oktoba, 2026 Milaadia.

Siku kama ya leo, kwa mujibu wa baadhi ya mapokezi ya kihistoria, miaka 838 iliyopita, yaani Oktoba Pili, 1187, mji wa Baitul-Muqaddas ulikombolewa na Salahuddin Ayyubi kamanda wa wanamapambano wa Kiislamu. Awamu ya kwanza ya vita vya Msalaba baina ya Wakristo na Waislamu ilianza 1096 ambapo miaka minne baadaye majeshi ya Msalaba yaliushambulia mji wa Baitul-Muqaddas na kuukalia kwa mabavu. Wanajeshi wao wa Msalaba walifanya uporaji na kuwaua kikatili maelfu ya wanawake, wanaume na watoto wasio na hatia wa ardhi hiyo. Hata hivyo mnamo mwaka 1187, baada ya Salahuddin Ayyubi kuidhibiti Syria, Lebanon na Misri, aliuzingira mji wa Baitul-Muqaddas. Awali aliwatumia ujumbe wavamizi akiwaeleza heshima maalumu anayoupa mji huo na kutotaka kufanya umwagaji damu katika eneo hilo na hivyo akawataka wavamizi hao waondoke katika mji huo na hata akawadhaminia usalama wa mali zao. Hata hivyo watu wa Msalaba walikataa na kupelekea kuibuka vita na mji huo kukombolewwa na Waislamu katika siku kama ya leo wakiongozwa na jemadari Salahuddin Ayyubi.

******

Katika siku hii miaka 313 iliyopita yaani mwezi 20 Mfunguo Saba Rabiuth-Thani 1134 Hijria, Alhajj Lotf-Ali Beyk Azar Bigdeli, mshairi na msomi wa fasihi kutoka Iran alizaliwa jijini Isfahan. Aliishi Qom na Shiraz kabla ya hatimaye kurejea na kuishi katika mji wake wa asili wa Isfahan baada ya kutekeleza ibada ya Hija. Licha ya njaa na ukosefu wa usalama uliosababishwa na vita nchini Iran wakati huo, hakuacha harakati zake za kutafuta elimu; alihudhuria mihadhara ya wasomi, washairi na watu wengi wenye maarifa na kunufaika na mafundisho ya kila mmoja wao. Alikuwa na ujuzi wa hali ya juu katika sanaa ya ushairi, uhakiki wa fasihi na maarifa kuhusu maisha na kazi za washairi. Miongoni mwa kazi zake muhimu ni mkusanyiko wa mashairi yake Diwani ya "Atashkadeh-ye Azar" (Hekalu la Moto la Azar), kitabu chenye mkusanyiko wa wasifu wa washairi wa zama zake pamoja na wale waliomtangulia.

*****

Miaka 157 iliyopita katika siku kama ya leo alizaliwa Mahatma Gandhi, kiongozi wa harakati ya kupigania uhuru nchini India katika moja ya vijiji vya jimbo la Gujarat. Mwaka 1891 Gandhi alirejea kutoka nchini Uingereza na kuishi mjini Mumbai. 1893 alisafiri kuelekea mjini KwaZulu-Natal nchini Afrika Kusini. Akiwa nchini humo Mahatma Gandhi alishuhudia ubaguzi wa rangi wa jamii ya wachache ndani ya taifa hilo. Mwaka 1917 na baada ya kurejea nchini kwake alipata umashuhuri mkubwa. Na miaka michache baada ya Vita vya Kwanza na vya Pili vya Dunia yaani akiwa na umri wa miaka 33 Gandhi aliongoza mapambano kwa ajili ya kuwaokoa watu wake sanjari na kupigania uhuru wa India kutoka mikononi mwa Waingereza ambapo hatimaye na baada ya kuvumilia matatizo mengi akiwa pamoja na shakhsia tofauti kama vile Jawaharlal Nehru akafanikiwa kulipatia uhuru taifa hilo mnamo mwaka 1947 Miladia.

****

Tarehe Pili Oktoba miaka 122 iliyopita alizaliwa Graham Greene mwandishi wa Uingereza. Mwandishi huyo aliakisi matendo mema na mabaya katika athari zake na aliandika kwenye kitabu chake kinachoitwa 'Nguvu na Utukufu' kwamba subira, uvumilivu na mateso ni njia ya wokovu. Graham Greene amealifu vitabu vingi na baadhi yao ni 'Mtu wa Tatu', 'Utawala Unaotisha' na Muuaji wa Kukodishwa'. Mwandishi huyo Muingereza alifariki dunia mwaka 1991.

****

Na miaka 68 iliyopita katika siku kama ya leo inayosadifiana na tarehe Pili Oktoba 1958, nchi ya Guinea Conakry ilipata uhuru kutoka kwa mkoloni Mfaransa. Wareno walianza kumiminika nchini Guinea mwishoni mwa karne ya 15, na mwanzoni mwa karne ya 19, Wafaransa walipata satua zaidi nchini humo. Mwaka 1849 nchi hiyo ilikoloniwa rasmi na Ufaransa. Guinea Conakry inapakana na nchi za Senegal, Mali, Ivory Coast, Liberia, Sierra Leone na Guinea Bissau.

******

Miaka 66 iliyopita yaani tarehe 20 Mfunguo Saba Rabiuth Thani, 1381 Hijria Ayatullah Hashem Modarres Qazvini, mwanachuoni wa Kiislamu na msomi mashuhuri, aliaga dunia. Alizaliwa mwaka 1270 Hijria karibu na Qazvin, magharibi mwa Iran na alianza masomo yake ya awali ya fiqhi, usuli na falsafa katika mji huo huo wa Qazvom. Baadaye, Ayatullah Qazvini alitumia miaka sita kusoma katika vyuo vya kidini vya Isfahan na baadaye Mash'had. Alifundisha mjini Mash'had kwa takriban miaka arubaini na kulea wanavyuoni kadhaa mashuhuri. Ayatullah Khamenei, Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu aliyeuawa shahidi tarehe 28 Februari 2026 Milaadi katika shambulio la kigaidi la Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel mjini Tehran, pia ni miongoni mwa wanachuoni waliopinda goti na kusoma kwa mwanachuoni huyo mkubwa. Ayatullah Sheikh Hashem Qazvini alikuwa mtu wa nidhamu ya kiroho, mwalimu wa daraja la juu mjini Mash'had, na mtu mwenye heshima kubwa na elimu ya kina, aliyejulikana sana miongoni mwa wanachuoni wakubwa wa mji huo na alikuwa mtu mwenye roho huru na mwenye mwanga mpana wa maarifa..."