Sep 30, 2026 06:02 UTC
  • Jumatano, 30 Septemba 2026

Leo ni Jumatano 18 Mfunguo Saba Rabiuthani 1448 Hijria mwafaka na 30 Septemba 2026 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 846 iliyopita, alizaliwa Abul Qasim Jafar bin Hassan Hilli maarufu kwa lakabu ya Muhaqiq Hilli, mmoja wa wanazuoni wakubwa na faqihi ya Kiislamu, katika mji mashuhuri wa Hillah, nchini Iraq. Muhaqiq Hilli alikuwa msomi aliyekuwa na nafasi ya juu na mtaalamu wa sheria za Kiislamu na alibobea pia katika fasihi na uandishi wa mashairi. Baada ya kukamilisha masomo ya awali na kupaa daraja za juu za kiroho, alitambuliwa kuwa miongoni mwa wanazuoni mashuhuri wa zama zake. Kitabu muhimu zaidi cha Muhaqqiq al Hilli ni Sharaiul Islam, fii Masaailil-Halal Walharaam'. Mwanazuoni huyo pia ameandika vitabu vya "Al Nafi", "Maarij" na "al Tanbih". Muhaqqiq al Hilli alifariki dunia mwaka 676 Hijria akiwa na umri wa miaka 74.

***

Siku ya leo ya tarehe 8 Mehr kwa mujibu wa kalenda ya Hijria Shamsia, ni maarufu hapa nchini Iran kama siku ya kumuenzi Maulana Jalaluddin Muhammad bin Bahauddin maarufu kwa jina la Moulavi. Maulana Jalaluddin alizaliwa mwaka 604 Hijria Qamaria katika mji wa Balkh uliokuwa moja kati ya miji ya Iran ya kipindi hicho. Moulavi alikuwa gwiji wa mashairi na malenga mwenye uwezo na kipaji kikubwa katika karne ya 7 Hijria. Miongoni mwa athari kubwa za Maulana au Jalaluddin Balkhi ni kitabu cha mashairi cha Masnavi Maanavi.  

***

Miaka 88 iliyopita katika siku kama ya leo ulifayika mkutano wa kihistoria wa Munich nchini Ujerumani. Mkutano huo ulihudhuriwa na Adolph Hitler na Benito Mussolini viongozi wa Ujerumani na Italia na pia Neville Chamberlain na Edouard Daladier, Mawaziri Wakuu wa wakati huo wa Ufaransa na Uingereza. Mkutano huo wa Munich ulifanyika kwa shabaha ya kutafuta njia ya kumaliza hitilafu kati ya Ujerumani na Czechoslovakia. Mkutano huo ulimalizika kwa kufikiwa makubaliano ya kuiunganisha sehemu moja ya ardhi ya Czechoslovakia na Ujerumani. 

***

Siku kama ya leo miaka 60 iliyopita yaani tarehe 30 mwezi Septemba mwaka 1966, nchi ya Botswana ilijipatia uhuru kutoka kwa mkoloni Muingereza. Botswana ilianza kukoloniwa na Uingereza mwaka 1885 Miladia. Harakati za wananchi wa Botswana za kuikomboa nchi yao zilishtadi tangu mwaka 1920 na kupelekea kupatikana uhuru wa nchi hiyo mwaka 1966. Nchi ya Bostwana iko kusini mwa bara la Afrika ikipakana na Afrika Kusini, Zimbabwe na Namibia.

***

Na Miaka 41 iliyopita, alifariki dunia mvumbuzi wa kipimo kinachotumiwa kupimia nguvu ya mtetemeko wa ardhi Charles Richter. Akishirikiana na mhakiki mwingine, Richter alipima mtetemeko huo kwa mujibu wa nishati inayotokana na mawimbi ya mitetemeko ya ardhi toka daraja moja hadi 9 na kusajili kipimo cha Rishta. Kabla ya hapo wataalamu walikuwa wakipima mitetemeko ya ardhi kwa kutegemea athari ya nje ya kipimo ambacho hakikuwa cha kuaminika. 

***