FAO yaonya kuhusu kumalizika fursa ya kuhuisha misitu
https://parstoday.ir/sw/news/world-i141820-fao_yaonya_kuhusu_kumalizika_fursa_ya_kuhuisha_misitu
Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) limeonya katika ripoti yake kwamba fursa ya kuhuisha misitu duniani, ambayo ina mchango mkubwa katika usalama wa chakula, inakaribia kumalizika.
(last modified 2026-09-30T02:50:03+00:00 )
Sep 30, 2026 02:48 UTC
  • FAO yaonya kuhusu kumalizika fursa ya kuhuisha misitu

Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) limeonya katika ripoti yake kwamba fursa ya kuhuisha misitu duniani, ambayo ina mchango mkubwa katika usalama wa chakula, inakaribia kumalizika.

Kwa mujibu wa Gazeti la The Guardian, Umoja wa Mataifa umeonya kwamba, muda wa dunia wa kurejesha misitu, ambayo ni muhimu kwa usalama wa chakula na kuimarisha uwezo wa kukabiliana na dharura ya mabadiliko ya tabianchi, unazidi kumalizika.

Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) limezitaka nchi duniani kuweka uhuishaji wa misitu kuwa kipaumbele cha kitaifa.

Kwa mujibu wa ripoti ya FAO, tangu mwaka 1990, zaidi ya hekta milioni 489 za misitu duniani zimepotea.

Ripoti hiyo inaeleza kwamba, ingawa hatua mbalimbali zimechukuliwa duniani za kulinda misitu na kupanda miti, lakini juhudi hizo bado hazijafikia kiwango kilichoahidiwa na nchi.

The Guardian inaongeza kuwa, katika kipindi cha miongo miwili iliyopita, mipango ya kitaifa, kikanda na kimataifa iliahidi kuhuisha zaidi ya hekta bilioni moja za misitu duniani. Hata hivyo, FAO inasema katika hali nzuri zaidi, ni moja ya tano tu (20%) ya ahadi hizo ambayo imetekelezwa.

Takwimu zinaonyesha kuwa kila mwaka karibu hekta milioni 127 za misitu huathiriwa na moto, wadudu, magonjwa na matukio makali ya hali ya hewa. Hali hiyo inazidi kuifanya misitu kuwa katika mazingira hatarishi.

Ripoti ya Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) pia imesisitiza kuwa kurejesha hekta bilioni moja za misitu kunaweza kuleta faida ya dola trilioni 1.8 kila mwaka.

Qu Dongyu, Mkurugenzi Mkuu wa FAO, amesema ripoti hiyo inaonyesha kuwa uhuishaji wa misitu na mandhari asilia si suala la kupewa kipaumbele kwa ajili ya mazingira pekee, bali ni uwekezaji wa kimkakati katika mifumo imara ya kilimo na chakula pamoja na maendeleo ya vijijini.

Ameongeza kuwa fursa ya kuchukua hatua inazidi kuwa finyu, na kuchelewesha uhuishaji wa misitu kutaongeza gharama za muda mrefu, kuzidisha ukosefu wa usawa na kuiweka dunia katika mwelekeo usio endelevu.