Alkhamisi, 16 Oktoba, 2025
Leo ni Alkhamisi tarehe 23 Mfunguo Saba Rabiuthani 1447 Hijria sawa na 16 Oktoba 2025 Miladia.
Miaka 848 iliyopita katika siku kama ya leo yaani tarehe 23 Rabiuthani mwaka 599 Hijria alizaliwa huko Damascus Shihabuddin Abdulrahman Dimashqi al-Maḳdisī maarufu kwa lakabu ya Abu Shama. Alikuwa mwanashistoria wa Kiarabu na alikuwa miongoni mwa walimu walioheshimika wa skuli za Damascus. Abdulrahman Dimashqi alielekea Alexandria nchini Misri baada ya masomo yake ya awali; na akiwa katika mji huo alijifunza hadithi, fiqhi na maarifa mengine ya zama hizo. Aidha kwa muda fulani alikuwa mkuu wa Darul Hadith Ashrafiyya.Vitabu kwa majina ya "Utangulizi wa Sarufi" na "Muhtasari mfupi wa Historia ya Damascus" ni miongoni mwa kazi za msomi huyo mkubwa.

Miaka 232 iliyopita katika siku kama ya leo yaani tarehe 16 mwezi Oktoba mwaka 1793 Malikia wa Ufaransa Marie Antoinette aliuawa kwa kukatwa kichwa kwa shoka kufuatia amri iliyotolewa na Baraza la Katiba la nchi hiyo na pia amri ya Maximilien Robespierre. Louis wa 16 aliyekuwa mume wa Antoinette miezi 10 kabla ya hapo alikuwa tayari amepatwa na hatma hiyo hiyo iliyomkuta mke wake. Marie Antoinette alikuwa binti wa Maria Theresa Walburga, mtawala wa Austria na Ufaransa. Antoinette aliolewa na Louis, mrithi wa kiti cha ufalme wa Ufaransa, mnamo mwaka 1770 akiwa na umri wa miaka 14. Hatua ya Louis ya kumuoa mwanamke huyo ilikuwa na nia ya kuzikurubisha pamoja nchi za Austria na Ufaransa ambazo wakati huo zilikuwa zikishindana barani Ulaya. Hata hivyo Wafaransa wengi hawakuridhia ndoa hiyo kiasi cha kuwafanya kuendelea kumwita ‘Muaustria’ hata kipindi alipokuwa tayari ni malikia wa Ufaransa.

Miaka 80 iliypita katika siku inayosadifiana na leo, liliasisiwa Shirika la Chakula Duniani (FAO). Hati ya kuasisiwa shirika hilo ilipasishwa Oktoba 16 mwaka 1945 katika mji wa Québec nchini Canada. Lengo ya kuasisiwa shirika la FAO ni kuzisaidia nchi wanachama kukusanya taarifa, ripoti na takwimu zinazohusiana na chakula, kilimo, utunzaji wa misitu na uvuvi na kufanya tathmini kuhusu uzalishaji wa chakula, ugavi wake na juhudi za kuboresha uzalishaji, masoko ya chakula, kulinda maliasili, kupanga sera zinazohusiana na kilimo na chakula na kadhalika. Siku hii pia inatambuliwa kuwa ni Siku ya Kimataifa ya Chakula.

Miaka 171 iliyopita mwafaka na tarehe 16 Oktoba mwaka 1854 Miladia, alizaliwa katika mji wa Dublin Oscar Wilde mwandishi mashuhuri wa Ireland. Oscar Wilde alipata elimu ya msingi katika mji wa Skyline kaskazini mwa Ireland na akajiunga na chuo kikuu cha Trinity na baadaye Oxford. Oscar Wilde alipata umaarufu baada ya kuandika mfululizo wa vitabu vya kisa cha Mwanamfalme Mwenye Furaha (The Happy Prince).

Na miaka 47 iliyopita katika siku inayosadiana na leo kulitokea maafa makubwa kwenye Msikiti Mkuu wa Kerman, huko magharibi mwa Iran baada ya polisi na askari usalama wa utawala wa mfalme Muhammad Reza Pahlavi kuwashambulia kwa risasi wananchi waliokusanyika kwenye eneo hilo la msikitini kwa shabaha ya kuwaenzi na kuwakumbuka mashahidi waliouawa tarehe 17 Shahrivar mjini Tehran. Idadi kubwa ya wananchi wasio na ulinzi waliuawa shahidi na kujeruhiwa katika hujuma hiyo. Shambulio hilo la askari usalama wa Shah liliamsha hasira na wimbi jipya la harakati za wananchi za kupinga utawala kibaraka wa Mfalme Muhammad Reza Pahlavi.
