Wanafunzi 185 wameuawa shahidi Iran katika hujuma za kigaidi za Israel, Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i137136-wanafunzi_185_wameuawa_shahidi_iran_katika_hujuma_za_kigaidi_za_israel_marekani
Waziri wa Elimu Iran, Alireza Kazemi, amesema katika mashambulizi ya kigaidi yaliyoanzishwa na Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Iran Jumamosi, hadi sasa wanafunzi wasiopungua 185 wameuawa shahidi.
(last modified 2026-03-04T02:23:39+00:00 )
Mar 04, 2026 02:23 UTC
  • Makaburi ya wanafunzi waliouawa katika hujuma ya Israel na Marekani wakiwa shuleni huko Minab, kusini mwa Iran
    Makaburi ya wanafunzi waliouawa katika hujuma ya Israel na Marekani wakiwa shuleni huko Minab, kusini mwa Iran

Waziri wa Elimu Iran, Alireza Kazemi, amesema katika mashambulizi ya kigaidi yaliyoanzishwa na Marekani na utawala wa Kizayuni wa Israel dhidi ya Iran Jumamosi, hadi sasa wanafunzi wasiopungua 185 wameuawa shahidi.

Aidha takriban shule 20 zimeshambuliwa kwa mabomu katika hujuma hizo za kigaidi za Israel na Marekani nchini. Kazemi amenukuliwa na Shirika la Utangazaji la Iran akisema: “Natuma salamu za rambi rambi kwa familia za wanafunzi na walimu  katika nchi nzima. Inaweza kuwa matukio kama haya hayajawahi kutokea katika historia ya binadamu.”

Kazemi aliendelea akisema: “Marekani na Israel hudai kutetea haki za binadamu lakini tawala hizo zimetekeleza hujuma ya kinyama dhidi ya wanafunzi wetu na walimu walipokuwa wakifundisha na kufundishwa ndani ya madarasa.”

Aidha amesema kuwa takriban wanafunzi na walimu 120 wamejeruhiwa na wako kwa sasa kwenye hospitali. Ameongeza kuwa, mashambulizi haya yamegusa shule, hospitali, huduma za dharura, na Shirika la Hilali Nyekundu na kuongeza kuwa jinai hizo ni ukiukaji mkubwa wa mikataba ya kimataifa. Hujuma mbaya zaidi dhidi ya shule ilijiri katika siku ya kwanza ya vita mjini Minab kusini mwa Iran katika shule ya wasichana ambapo wanafunzi wasiopungua 167 walijeruhiwa.

Wakati huo huo, Volker Türk Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa ametaka ufanyike uchunguzi wa haraka kuhusu shambulio la kinyama lililofanywa katika siku ya kwanza ya uchokozi wa pamoja wa kijeshi wa Marekani na utawala wa kizayuni wa Israel dhidi ya shule hiyo ya msingi.

Wakati huohuo msemaji Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Ravina Shamdasani amesema, shambulio hilo lililofanywa wakati wa masomo wanafunzi wakiwa madarasani ni la umwagaji mkubwa zaidi wa damu na la uharibifu mkubwa zaidi katika machafuko ya karibuni.