Seneta wa Marekani: Vita vimeifanya Iran kuwa imara zaidi, Marekani imedhoofika
-
Seneta Chris Murphy wa jimbo la Connecticut katika Seneti ya Marekani
Seneta mmoja wa Marekani, amekiri wazi kushindwa serikali ya Donald Trump katika vita dhidi ya Iran, na kubainisha kwamba, vita hivyo vimesababisha Marekani kudhoofika na Iran kuwa na nguvu zaidi.
Seneta Chris Murphy wa jimbo la Connecticut katika Seneti ya Marekani, akikiri madhara ya vita dhidi ya Iran kwa nchi yake, amesema yuko tayari kuunga mkono makubaliano yoyote yatakayomaliza vita hivyo, hata kama yatakuwa ni makubaliano “mabaya”.
Murphy amesema gharama zinazotokana na kuendelea vita zinaongezeka, huku Marekani ikiendelea kukabiliwa na athari zake. Ameongeza kuwa wananchi wa Marekani wanateseka kutokana na vita hivyo, na gharama za kufunguliwa tena Lango Bahari la Hormuz zinaongezeka siku hadi siku.
Seneta huyo wa Marekani amesema pia kuwa, Trump ameshindwa katika vita hivyo, na kwamba matokeo yake ni kudhoofika Marekani huku Iran ikiwa imekuwa na nguvu zaidi.
Vita dhidi ya Iran vimezidi kuwa vita vinavyochukiza ndani ya Marekani, na wabunge wa Kongresi ya nchi hiyo kutoka vyama vyote viwili vya siasa vya vya Republican na Democratic wamekatishwa tamaa na serikali yao
Hayo yanaripotiwa siku moja tu baada ya Mkuu wa Majeshi ya Marekani, Jenerali Daniel Caine, kuwasihi maafisa wakuu wa utawala wa Trump kutafuta njia ya kupunguza vita na Iran, akionya kwamba ongezeko zaidi la mapigano ya kijeshi haliwezi kupata mafanikio makubwa na kwamba linawaweka wanajeshi wa Marekani na washirika wake katika hatari ya majibu angamizi ya Iran.
Wakati huo huo, idadi kubwa ya wapiga kura nchini Marekani wanaamini kuwa vita vya Donald Trump dhidi ya Iran havijazalisha tija inayostahili gharama zilizotumika. Kulingana na utafiti mpya wa gazeti la Financial Times, hali hiyo inaashiria jinsi mzozo huo unavyozidi kudhoofisha uungaji mkono kwa mtawala huyo kuelekea uchaguzi wa katikati wa muhula mwezi Novemba.