Kwa nini ni lazima Marekani iondoke Asia Magharibi?
https://parstoday.ir/sw/news/west_asia-i140582-kwa_nini_ni_lazima_marekani_iondoke_asia_magharibi
Uwepo wa kijeshi wa Marekani katika eneo la Asia Magharibi, ambao kwa miaka mingi umehalalishwa kwa kisingizio cha kudhamini usalama, sasa umekuwa kichocheo cha migogoro, sababu ya kuongezeka gharama, na jambo linaloitumbukiza Washington katika vita vya kuchosha na vya muda mrefu, kuliko wakati mwingine wowote.
(last modified 2026-08-11T08:02:41+00:00 )
Aug 11, 2026 07:54 UTC
  • Kwa nini ni lazima Marekani iondoke Asia Magharibi?

Uwepo wa kijeshi wa Marekani katika eneo la Asia Magharibi, ambao kwa miaka mingi umehalalishwa kwa kisingizio cha kudhamini usalama, sasa umekuwa kichocheo cha migogoro, sababu ya kuongezeka gharama, na jambo linaloitumbukiza Washington katika vita vya kuchosha na vya muda mrefu, kuliko wakati mwingine wowote.

"Vikosi vya Marekani katika eneo la Asia Magharibi si tu kwamba vimeshindwa kudhamini usalama, bali vyenyewe vimekuwa chanzo kikuu cha ukosefu wa utulivu na vita vya gharama kubwa. Hivyo wakati wa kuondoka umewadia." Maneno haya yanafupisha ripoti ya hivi karibuni ya jarida la Foreign Affairs kuhusu mustakabali wa uwepo wa kijeshi wa Marekani katika eneo la Asia Magharibi, ripoti inayoonyesha kuwa baadhi ya wadau wa masuala ya kimkakati mjini Washington hawachukulii tena uwepo mkubwa wa kijeshi wa Marekani kama chombo cha kudhamini usalama, bali wanaona uwepo huo kama chanzo cha ukosefu wa utulivu na ongezeko la gharama, pamoja na sababu inayoiingiza nchi hiyo katika vita vya kuchosha na vya muda mrefu.

Vitendo vya hivi karibuni vya uchokozi wa kijeshi dhidi ya Iran, vilivyoitwa na Foreign Affairs kama "Maafa kamili", vimeweka wazi zaidi kuliko wakati mwingine wowote, mgongano wa misimamo iliyopo mjini Washington kuhusiana na suala hili. Katika miongo kadhaa iliyopita, Marekani ilijitahidi kudhibiti uwiano wa nguvu katika Mashariki ya Kati kwa kuanzisha mtandao mpana wa kambi za kijeshi, kutuma askari, kudumisha uwepo wa vikosi vya majini na anga, na kutoa ahadi za kudhamini usalama. Hata hivyo, madai hayo hayakumaliza migogoro, bali yaliibua migogoro zaidi ambayo gharama zake za kibinadamu, kifedha na kimkakati, mara nyingi, zimezidi faida zilizopatikana kwa maslahi ya Washington.

Moja ya hoja kuu zinazotolewa kuhalalisha uwepo wa Marekani katika Ghuba ya Uajemi ni hitaji la kulinda mtiririko wa nishati na kuhakikisha uhuru wa usafiri wa majini katika Lango-Bahari la Hormuz. Hata hivyo, vita vya karibuni vimefichua mgongano mkubwa uliopo katika hoja hiyo. Hatua ya kijeshi iliyochukuliwa na Marekani na utawala wa Kizayuni dhidi ya Iran, kwa madai ya kuhakikisha usalama, hatimaye yenyewe imepelekea kufungwa kwa hilo, ambapo jeshi la Marekani limeshindwa kulifungua tena kwa kutegemea nguvu zake za kijeshi. Uzoefu huu unathibitisha wazi kuwa uwepo wa kijeshi haumaanishi moja kwa moja usalama zaidi, bali wakati wa mzozo, vikosi na kambi za Marekani vyenyewe vinaweza kuwa shabaha ya mashambulizi na hata kupanua wigo wa mgogoro.

Hoja nyingine muhimu katika ripoti ya jarida la Foreign Affairs ni kwamba hata uamuzi wa kupunguza uwepo wa kijeshi wa Marekani hautatatua tatizo hilo moja kwa moja, kwani kubakisha hata kambi moja au mbili za kijeshi bado kunaweza kuzifanya kambi hizo kuwa shabaha kuu ya mashambulizi katika mzozo wowote wa siku zijazo.

Mapigano ya hivi karibuni pia yameithibitishia wazi Marekani ukweli huo mchungu. Mashambulizi ya Iran dhidi ya kambi na vituo vya Marekani katika eneo yameonyesha kuwa mtandao mpana wa vikosi vya kijeshi ingawa una faida za kiutendaji, lakini pia unafungamana na gharama kubwa na hatari za kushambuliwa kirahisi. Ili kulinda vituo hivi, Marekani inalazimika kutenga rasilimali zaidi kwa ajili ya mifumo ya ulinzi wa anga, usafirishaji na ugavi pamoja na wafanyakazi. Kadiri mvutano unavyoongezeka, ndivyo gharama za kudumisha mtandao huu zinavyoongezeka pia.

Suala hili linapata uzito zaidi wakati ongezeko la matumizi ya kijeshi ya Marekani linapotiliwa maanani. Bajeti ya Pentagon mwaka huu wa 2026 tayari imefikia takriban dola trilioni moja, huku ripoti zikikadiria kuwa gharama za operesheni za kivita zinafikia mamia ya mamilioni ya dola kwa siku. Hata hivyo, gharama halisi za uwepo wa jeshi la Marekani Asia Magharibi ni zaidi ya takwimu za kifedha pekee. Rasilimali na uwezo uliotumika katika eneo hili vingeweza kutumika kwa ajili ya kukabiliana na ushindani wa kimkakati na China, kuimarisha usalama wa Ulaya na kuendeleza teknolojia ya kisasa nchini Marekani. Sambamba na mahesabu haya ya kimkakati na kiuchumi, mabadiliko makubwa katika maoni ya umma nchini Marekani pia yanaendelea kujitokeza. Kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Foreign Affairs, asilimia 62 ya Wamarekani wanapendelea nchi yao ijiepushe na vita kadiri inavyowezekana, huku asilimia 33 pekee wakiafiki matumizi ya nguvu za kijeshi katika kutetea maslahi ya Marekani.

Upinzani mkubwa wa kizazi cha vijana dhidi ya vita na Iran pia unaashiria mabadiliko ya kimtazamo kati ya vizazi tofauti kuhusiana na uingiliaji wa Marekani katika masuala ya ndani ya nchi nyingine. Baada ya kushuhudia vita vya Iraq na Afghanistan, Wamarekani sasa wanahoji zaidi uhusiano uliopo kati ya gharama za vita na faida zake halisi, kuliko ilivyokuwa katika miaka ya nyuma. Kwa muda mrefu, mabadiliko haya yanayoendelea katika maoni ya umma yanaweza kuwa kikwazo kikubwa katika siasa za ubeba za Washington za kuingilia masuala ya ndani ya mataifa mengine. Kwa hakika, changamoto kubwa inayoikabili Washington leo sio tena "namna ya kuidhibiti Asia Magharibi," bali zaidi ni jinsi ya kulinda maslahi ya Marekani bila kujihusisha tena na migogoro ya kikanda.

Ripoti ya jarida la Foreign Affairs ni muhimu katika muktadha huu. Haipendekezi tu kupunguzwa kwa vikosi vya Marekani, bali inahoji dhana ya muda mrefu ya kiusalama, iliyojengeka juu ya imani kwamba uwepo wa kudumu wa kijeshi wa Marekani katika eneo ungeweza kudhamini utulivu wa kudumu Mashariki ya Kati.

Iwapo hatimaye Washington itaamua kuondoa majeshi yake Asia Magharibi, hatua hiyo haitahusu tu suala la kuhamisha au kurudisha nyuma vikosi vya kijeshi, bali itaashiria mwisho wa zama maalum za kijiopolitiki na kuanza kwa awamu mpya ambapo jukumu la kudhamini usalama wa eneo litakabidhiwa kwa wadau halisi wa eneo badala ya kutegemea wageni wenye tamaa ya kupora utajiri wa mataifa ya eneo hili.

Kwa mtazamo huu, kufukuzwa Marekani Asia Magharibi mbali na kuashiria kushindwa kijeshi, kutaashiria pia mabadiliko muhimu katika mfumo wa usalama wa eneo na kupungua taratibu kwa nafasi yake kama nguvu kuu yenye ushawishi mkubwa katika eneo.