Iran: Haya ndiyo masharti yetu ya kufungua Lango Bahari la Hormuz
Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran ametangaza kuwa kufunguliwa upya Lango Bahari la Hormuz kunategemea Marekani kurejea na kuheshimu ahadi zake chini ya Mkataba wa Maelewano wa Islamabad.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Tasnim, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran, Sayyid Abbas Araghchi amesema hayo katika mahojiano maalumu na Al-Araby Al-Jadeed kuhusu mkutano uliokuwa umepangwa kufanyika leo Jumatatu wa nchini Oman na kusisitiza kuwa, ajenda ya mkutano huo ulioakhirishwa ilihusu njia mpya ya usafiri wa baharini katika Lango Bahari la Hormuz.
Araghchi amefafanua zaidi kwa kusema: "Makubaliano yetu na Oman hayamaanishi hata kidogo kufunguliwa upya Lango Bahari la Hormuz. Sharti la Iran la kufungua tena Lango hilo ni Marekani kutekeleza wajibu wake chini ya Mkataba wa Maelewano wa Islamabad."
Waziri wa Mambo ya Nje pia amesema: "Iran inaamini kuwa jukumu la kuhakikisha usalama na utulivu wa eneo hili liko mikononi mwa nchi zenyewe za eneo hili si madola kutoka nje."
Ameongeza kwamba: "Tunatumai kuona kuwa mazungumzo yetu na Oman yatafungua njia ya mashauriano ya baadaye kuhusu masuala yenye maslahi ya pamoja kwa nchi zote za eneo hili."
Kabla ya hapo pia, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran alikuwa amesisitiza kuwa Lango Bahari la Hormuz litaendelea kuwa chini ya udhibiti kamili wa Iran, akisema kwamba, Marekani ndiye wa kulaumiwa kwa kuvurugika usalama wa baharini wa eneo hilo na inapasa ilaumiwe pia kwa kupanda bei ya mafuta duniani.